Jamaa apatikana ameuawa katika nyumba ya wageni Machakos, kondomu zilizotumika zapatikana

Muhtasari

•Marehemu aliingia ndani ya chumba hicho mwendo wa saa mbili usiku wa Jumatatu akiwa ameandamana na mwanamke ambaye bado hajatambulika.

crime scene 1
crime scene 1
Image: HISANI

Wapelelezi katika kaunti ya Machakos wanachunguza mauaji ya jamaa mmoja ambaye alipatikana amefariki katika nyumba ya wageni iliyo eneo la Mlolongo.

Mwili wa Clinton Wanakacha ,26, ulipatikana asubuhi ya Jumanne ukiwa umetandazwa kitandani katika chumba nambari sita cha Nyumba ya Wageni ya Miathathia .

Kitengo cha upelelezi wa Jinai (DCI) kimeripoti kwamba mipira miwili ya kondomu ambayo ilikuwa imetumika ni baadhi ya vitu vilivyopatikana katika eneo la tukio.

Mfanyikazi mmoja katika nyumba hiyo ya wageni alifahamisha wapelelezi kwamba marehemu aliingia ndani ya chumba hicho mwendo wa saa mbili usiku wa Jumatatu akiwa ameandamana na mwanamke ambaye bado hajatambulika.

Wapelelezi waliofika katika eneo la tukio walichunguza chumba hicho kwa kina ili kupata ushahidi ambao ungesaidia kumtambua mtuhumiwa wa mauaji hayo.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City Mortuary huku uchunguzi zaidi ukiendelea.