Polisi wamsaka mwanamke aliyewadunga kisu wanawe 2 Murang'a, 1 aaga dunia

Muhtasari
  • Mtoto 1 afariki, mwingine auguza majeraha baada ya kudungwa kisu na mama
  • Mkurugenzi wa DCI George Kinoti alisema Jumatatu kwamba Munjiro ni mama asiye na mwenzi wa watoto wawili; mtoto wa miaka minne na mwenye miaka miwili
Crime scene
Crime scene

Polisi wameanzisha msako wa kumsaka mama anayeshukiwa kuwa muuaji aliyewadunga kisu watoto wake wawili katika kijiji cha Kianjogu huko Kahuro na kumuua mmoja papo hapo.

Nancy Munjiro 21, aliwageuzia watoto wake kisu cha muuaji katika nyumba ya nyanya yao.

Mkurugenzi wa DCI George Kinoti alisema Jumatatu kwamba Munjiro ni mama asiye na mwenzi wa watoto wawili; mtoto wa miaka minne na mwenye miaka miwili.

Kinoti alisema mtoto huyo wa miaka miwili alifariki papo hapo na kuongeza kuwa mkubwa alikimbizwa katika hospitali ya Muriranjas kabla ya kupewa rufaa katika hospitali ya Kaunti ya Murang'a akiwa katika hali mbaya.

"Kile ambacho nyanya wa watoto alitarajia kingekuwa wakati muhimu wa uhusiano kati ya mama na wanawe alipotoka nyumbani kwake asubuhi, na ikawa siku yenye giza zaidi kwake," Kinoti alisema.

"Alirudi tu na kukuta nyumba yake imegeuzwa kuwa eneo la mauaji, wajukuu zake wakiwa wamelowa damu na wametapakaa sakafuni."

Munjiro, ambaye anafanya kazi kama msaidizi wa nyumba katika eneo la Kiriaini, Kahuro, alikuwa amemtembelea mamake wakati wa msimu wa sherehe na alikuwa bado kuripoti mahali pake pa kazi.

Polisi waliotembelea eneo la tukio pia walipata kamba ikining'inia juu ya paa, wakishuku kuwa huenda mshukiwa alijaribu kujiua kabla ya kukimbia.