Shule zafunguliwa Uganda baada ya miaka 2

Muhtasari

• Wanafunzi wapatao milioni 15 hawajahudhuria shule nchini Uganda tangu Machi 2020 wakati madarasa yalipofungwa huku Covid-19 ikienea ulimwenguni. 

• Mashirika ya kutetea haki za watoto yamekosoa uamuzi wa Uganda wa kufunga shule kikamilifu au kwa sehemu kwa muda wa wiki 83, muda mrefu zaidi kuliko mahali pengine popote duniani.

• Uganda imerekodi visa 153,762 vya Covid-19 na vifo 3,339, kulingana na takwimu za hivi punde za serikali zilizotolewa Januari 7.

Wanafunzi wapatao milioni 15 hawajahudhuria shule nchini Uganda tangu Machi 2020 wakati madarasa yalipofungwa huku Covid-19 ikienea ulimwenguni. Picha: UNICEF Uganda/2021/Abdul
Wanafunzi wapatao milioni 15 hawajahudhuria shule nchini Uganda tangu Machi 2020 wakati madarasa yalipofungwa huku Covid-19 ikienea ulimwenguni. Picha: UNICEF Uganda/2021/Abdul

Uganda hatimaye siku ya ilisitisha muda mrefu zaidi duniani kwa shule kufungwa.Serikali ya rais Yoweri Museveni iliamuru mamilioni ya wanafunzi kurudi shuleni takriban miaka miwili baada ya kusimamishwa kwa shughuli za masomo nchini humo kwa sababu ya janga la coronavirus. 

Wanafunzi wapatao milioni 15 hawajahudhuria shule nchini Uganda tangu Machi 2020 wakati madarasa yalipofungwa huku Covid-19 ikienea ulimwenguni. 

Waziri wa Elimu John Muyingo alisema wanafunzi wote watarejelea masomo mwaka mmoja juu ya kiwango walichokuwa kabla ya shule kufungwa.  

"Shule zote zimetekeleza miongozo na taratibu za kawaida za uendeshaji ili kuhakikisha watoto wanarudi salama shuleni, na hatua zimewekwa kuhakikisha wale ambao hawatatii wanafanya hivyo," aliiambia AFP. 

Muyingo alisema shule zozote za kibinafsi zinazodai ada zaidi ya viwango vya kabla ya janga zitaadhibiwa. Harakati za kuwarudisha watoto shuleni zilisababisha msongamano wa magari katika mji mkuu Kampala. 

Mashirika ya kutetea haki za watoto yamekosoa uamuzi wa Uganda wa kufunga shule kikamilifu au kwa sehemu kwa muda wa wiki 83, muda mrefu zaidi kuliko mahali pengine popote duniani.

 "Hatuwezi kuruhusu hili kutokea tena. Ni lazima tuweke shule wazi kwa kila mtoto, kila mahali," shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za watoto UNICEF lilisema kwenye Twitter. 

Shirika la hisani la Save the Children lilisema wanafunzi wangetatizika kubadilika baada ya kuwa nyumbani sana, na kuonya kuwa kunaweza kuwa na viwango vya juu vya kuacha shule katika wiki zijazo bila uingiliaji wa haraka wa kusaidia wanafunzi. 

Uganda imerekodi visa 153,762 vya Covid-19 na vifo 3,339, kulingana na takwimu za hivi punde za serikali zilizotolewa Januari 7.