Sankok kuwasilisha kesi kumzuia Raila kuania urais

Muhtasari

• Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, Sankok alisema ana kundi la mawakili walio tayari kuwasilisha kesi mahakamani kuhusu madai hayo ya uhaini.

• Wakati wa kiapo cha dhihaka 2017, Mwanasheria Mkuu wa wakati huo Githu Muigai alisema adhabu ya kufanya uhaini ni kifo.

• Miaka miwili baadaye, mahakama ilisema kuwa kuapishwa kwa Raila si haramu.

Sankok
Sankok

Mbunge maalum David Sankok anataka kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga azuiwe kuwania kiti cha urais akidai amefanya uhaini mara mbili.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, Sankok alisema ana kundi la mawakili walio tayari kuwasilisha kesi mahakamani kuhusu madai hayo ya uhaini.

“Raila alifanya uhaini 1982 na pia alijiapisha 2017. Waliomwapisha waliadhibiwa, ilhali Raila hajaadhibiwa,” alisema.

"Je, ni kwa sababu ya Handshake? Je, Handshake huosha dhambi zako zote?" alisema.

Wakati wa kiapo cha dhihaka 2017, Mwanasheria Mkuu wa wakati huo Githu Muigai alisema adhabu ya kufanya uhaini ni kifo.

kinara wa ODM Raila Odinga
kinara wa ODM Raila Odinga
Image: Hisani

“Kuapishwa kwa mtu yeyote ambaye hakutangazwa na IEBC, na ambaye hakushinda uchaguzi, hakukubaliki,” akasema.

Githu pia alibainisha kuwa ikiwa kiapo hakifanywi na Jaji Mkuu ni batili na haramu.

Lakini miaka miwili baadaye, mahakama ilisema kuwa kuapishwa kwa Raila si haramu.

Hakimu Mkuu Stephen Mbungi alisema kuwa kiapo kilichochukuliwa baada ya uchaguzi wa urais uliozozaniwa wa 2017 si kinyume cha sheria na kwamba angewajibishwa tu ikiwa angetumia kiapo chake kutekeleza uhalifu.