Spika Muturi apuuzilia mbali mazungumzo ya muungano na OKA

Muhtasari

• Muturi alisema vinara wa Oka walimtembelea ili kumtakia heri kufuatia upasuaji wake.

Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Image: WILFRED NYANGARESI

Spika wa Bunge Justin Muturi amepuuzilia mbali ripoti kwamba anafanya mazungumzo ya muungano na vinara wa One Kenya Alliance (OKA).

Alipokuwa anahutubia wanahabari baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la chama cha Democratic Party (DP) katika hoteli ya Nairobi, Muturi alisema vinara wa Oka walimtembelea ili kumtakia heri kufuatia upasuaji wake.

"Uamuzi wa mimi kushirikisha vyama vingine katika mazungumzo ya muungano unaweza tu kufanywa na chombo cha juu cha kufanya maamuzi cha DP. Siwezi kufanya uamuzi huo kama mtu binafsi," Muturi alisema.

Pamoja naye alikuwa kiongozi wa chama Francis Munyao na maafisa kutoka matawi mbalimbali ya chama hicho.

Munyao alisema chama hicho kitatangaza Kongamano la Wajumbe la Kitaifa baadae wiki hii ambapo masuala ya muungano yatajadiliwa.

"Tutamwidhinisha Muturi kama mgombeaji wetu wa urais na kujadili masuala kuhusu kuungana na vyama vyenye nia kama hiyo," alisema.

Munyao alisema DP itafanya mkutano wake wa NDC kabla ya mwisho wa Februari.