Inspekta wa polisi atiwa mbaroni kwa kudai hongo Thika

Muhtasari

• Inspekta David Simiyu kutoka kituo cha polisi cha Kikuyu alinusurika kifo baada ya maafisa wenzake waliokuwa wakishika doria kumpata akipigwa na umati wenye hasira kwa kudai hongo kutoka kwa mhudumu wa duka la kuuza pombe.

• Mathenge alisisitiza kwamba yeye ni mfanyibiashara halali, jambo ambalo halikumpendeza Simiyu pamoja na wenzake wakajaribu kumtia pingu.

Inspekta wa polisi akamatwa kwa kudai hongo Thika
Inspekta wa polisi akamatwa kwa kudai hongo Thika
Image: TWITTER/ DCI

Afisa wa polisi wa cheo cha inspekta amewekwa kizuizini baada ya kuokolewa kutoka kwa umati wa watu wenye ghadhabu waliotaka kumuua kwa kuitisha hongo.

Inspekta David Simiyu kutoka kituo cha polisi cha Kikuyu alinusurika kifo baada ya maafisa wenzake waliokuwa wakishika doria kumpata akipigwa na umati wenye hasira kwa kudai hongo kutoka kwa mhudumu wa duka la kuuza pombe.

Kitengo cha upelelezi wa jinai (DCI) kimeripoti kwamba Simiyu alikuwa ameandamana na watu wengine wawili hadi duka la Heisenberg Wines and Spirit wakijifanya maafisa wa KRA na kuanza kuhangaisha mwenye duka aliyetambulishwa kama David Mathenge.

Simiyu na wenzake walimshtumu Mathenge kwa kukosa kuwapa wateja wake risiti ya kodi ya ETR na kuuza pombe zilizo na muhuli bandia.

Baada ya kumsingizia Mathenge makosa hayo, maafisa hao bandia walimwagiza atoe kiasi kikubwa cha hongo, agizo ambalo alikaidi.

Wakati hayo yote yalikuwa yakiendelea kikundi cha vijana ambao hubangaiza karibu na duka hilo walikuwa wanatazama kwa hasira.

Mathenge alisisitiza kwamba yeye ni mfanyibiashara halali, jambo ambalo halikumpendeza Simiyu pamoja na wenzake wakajaribu kumtia pingu.

Mfanyibiashara huyo alipatwa na hisia kwamba maafisa wale walikuwa wakora waliokusudia  kumwibia na hapo akaanza kuita usaidizi.

Nduru za Mathenge zilijibiwa na kikundi cha vijana ambao walifika pale na kuwafurusha maafisa hao bandia. Wawili wao waliweza kutoroka kwa gari ila Simiyu akapatikana na kupewa kichapo cha mbwa.

Kwa bahati maafisa waliokuwa karibu waliweza kumwokoa  kabla hajaangamizwa kisha wakampeleka kituoni. 

Baada ya mahojiano ilibainika kwamba Simiyu ni polisi mkora na tayari anakabiliwa na kesi zingine tatu za ulaghai.

Kitambulisho bandia cha KRA kilipatikana mifukoni yake. Simiyu anaendelea kuzuiliwa kituoni akisubiri kushtakiwa  kwa kosa la uigaji na kughushi.