Mzozo wa ugavi wa mali ya hayati Moi waelekea mahakamani

Muhtasari

• Mmoja wa wajukuu wa Moi mwanawe Jonathan Moi (marehemu) – anasema kwenye nyaraka za mahakama kwamba thamani halisi ya utajiri wa babu yake ni zaidi ya Shilingi bilioni 300.

• Collins Kibet Toroitich Moi anasema mali ya babu yake, ambayo anaiita "kubwa", imeenea duniani kote, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Australia na Malawi.

• Watoto wa marehemu Moi ni pamoja na Jonathan Kipkemboi, Raymond, John Mark, Philip na Gideon.

Hayati rais mustaafu Daniel Arap Moi
Hayati rais mustaafu Daniel Arap Moi
Image: HISANI

Mali ya aliyekuwa Rais Daniel Moi umefichuliwa kwa mara ya kwanza katika mzozo wa kugawana mali yenye thamani ya mabilioni ya pesa mahakamani.

Mmoja wa wajukuu wa Moi—mtoto mkubwa wa kwanza wa Jonathan Moi (marehemu) – anasema kwenye nyaraka za mahakama kwamba thamani halisi ya utajiri wa babu yake ni zaidi ya Shilingi bilioni 300.

Daima kumekuwa na maswali mengi kuhusu Moi anamiliki nini hasa, baada ya kuhudumu kama rais kwa kipindi cha miaka 24 na miaka 11 kama makamu wa rais.

Collins Kibet Toroitich Moi anasema mali ya babu yake, ambayo anaiita "kubwa", imeenea duniani kote, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Australia na Malawi.

Kibet amekwenda mahakamani akidai njama ya kumnyima urithi kama mrithi wa mali ya Moi na anamlaumu wakili Zehrabhanu Janmohamed, msimamizi na mdhamini wa wosia wa Moi, kwa masaibu yake.

“Msimamizi amejaribu kwa nia mbaya na isiyo halali kuninyima urithi na kunilaghai sehemu yangu ya manufaa ya mirathi ya marehemu kwa kunitenga kimakusudi kama mnufaika wa mirathi ya marehemu, licha ya nyakati zote kujua kwamba mimi ndiye mrithi wa mali ya marehemu. Mjukuu wa marehemu,” Kibet anasema kwenye stakabadhi zilizopatikana mahakamani na Star.

Anadai kuwa Janmohamed huchukua tu maagizo kutoka kwa mrithi mmoja ambaye hakumtaja.

"Msimamizi anaonekana kuchukua maagizo kutoka kwa mhusika mmoja na asiyejulikana licha ya ukweli kwamba anapaswa kuwashirikisha warithi wote wa mali nikiwemo mimi kwa njia ya haki na uwazi," anasema kwenye stakabadhi za madai.

Kibet anadai Janmohamed anatoa mali ya Moi bila idhini, akitoa mfano wa Siginion Group.Siginon ni kampuni ya kutoa huduma jumuishi za vifaa na mizigo kupitia angani inayoendesha shughuli zake nchini Kenya, Tanzania na Uganda. 

Anasema hisa za kampuni hiyo kitengo cha ndege ziliuzwa kwa Shilingi bilioni 1.7. 

"Msimamizi amethibitisha kuwa hawezi kuaminiwa kusimamia mali za marehemu pekee...Janmohamed ameshindwa kueleza hali ya mapato hayo ya mauzo ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.7 licha ya maombi mbalimbali ya mlalamishi. ” anasema. 

Kwa mara ya kwanza, pia anafichua kwamba Moi alikuwa na ekari 1,000 za ardhi inayojulikana kama Kimintet A. No.1, ambayo anasema pia imetengwa kuuzwa. 

“Majengo yanayojulikana kwa jina la Kimintet A No.1 yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 1,000 kwa sasa yako kwenye mchakato wa kuuzwa kinyume cha sheria na kwa  siri kwa mtu wa tatu kabla ya ruzuku ya hati ya uthibitisho iliyopingwa kuthibitishwa na mahakama kama inavyotakiwa kisheria,” anahoji. 

Ardhi ya Kimintet inaaminika kuwa katika kaunti ya Narok. Kibet sasa anaitaka mahakama kutoa maagizo ya haraka kumzuia msimamizi kushughulikia mali ya Moi.

 "Kuna hatari ya kweli kwamba ikiwa amri za muda hazitatolewa haraka kuzuia shughuli zozote zaidi za msimamizi wa mirathi na mali ya marehemu, kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa wito huu, kesi hizi zitafanywa kuwa zoezi la kitaaluma tu," anasema. 

Familia ya Moi pia inamiliki hekta 931 zinazomilikiwa na wadhamini wa Chuo Kikuu cha Kabarak.Katika wosia wake, ambao pia uliwasilishwa kortini, marehemu Rais Moi aligawana mali yake kwa usawa kati ya wanawe watano na ikiwa mtoto yeyote ameaga kama ilivyo na familia Jonathan, watoto wao wangepewa urithi. 

Watoto wa marehemu Moi ni pamoja na Jonathan Kipkemboi, Raymond, John Mark, Philip na Gideon. Kibet anataka, miongoni mwa mambo mengine, hesabu sahihi ya mali na madeni ya Moi na kuondolewa kwa mamlaka aliyopewa wakili Janmohammed kusimamia mali ya Moi. 

Janmohamed alipewa mamlaka ya kusimamia mali ya Moi mnamo Oktoba 9, 2020 baada ya kifo cha Rais huyo wa zamani mnamo Februari 4 mwaka huo huo.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO