Wafungwa katika gereza la Kamiti waandamana kupinga hatua mpya za kuwaadhibu

Muhtasari

•Wafungwa hao walilalamika kuwa hawawezi kufungiwa ndani mchana na usiku kwa sababu tu wafungwa watatu kati yao walitoroka kutoka gerezani.

Picha ya gereza ya Kamiti
Picha ya gereza ya Kamiti
Image: PATRICK VIDIJA

Mnamo Alhamisi baadhi ya wafungwa katika gereza ya Kamiti Maximum  walishiriki maandamano kulalamikia hatua mpya kali za kuwaadhibu zilizoletwa na mamlaka.

Mtoa habari mmoja alitufichulia kwamba wafungwa hao walilalamika kuwa hawawezi kufungiwa ndani mchana na usiku kwa sababu tu wafungwa watatu kati yao walitoroka kutoka gerezani.

Wafungwa hao wanasema wamedhulumiwa kufuatia kutoroka kwa wafungwa watatu wa kigaidi miezi miwili iliyopita na sasa wangependa kuhurumiwa.

Kanda za video ya drama iliyojitokeza pale Alhamisi ambayo inaonyesha wafungwa hao wakiwa wamepiga kambi kwenye paa la majengo ya magereza wakionekana wenye hasira.

Siku ya Jumanne PS mpya Safina Kwekwe alizuru gereza hilo kutathmini maendeleo ya kituo hicho tangu kutoroka tatanishi kwa wafungwa watatu wa kigaidi mnamo mwezi Novemba.

Wafungwa hao watatu ni pamoja na Musharaf Abdalla, ambaye alipatikana na hatia ya kujaribu kushambulia bunge mwaka 2012; Joseph Juma Odhiambo, ambaye alikamatwa mwaka wa 2019 katika mpaka wa Kenya na Somalia kwa kupanga kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabab; na Mohamed Abdi Abikar, ambaye alitiwa hatiani kwa kuhusika katika shambulio la al-Shabab kwenye Chuo Kikuu cha Garissa mnamo Aprili 2015.

Kutoroka kwa wafungwa hao kulipelekea kufutwa kazi kwa mkuu wa magereza na kukamatwa kwa walinzi 13 wa gereza hilo.

Rais Uhuru Kenyatta alifanya mabadiliko makubwa katika idara ya magereza ikiwemo kufutwa kazi kwa Wycliffe Ogalo kama Kamishna Mkuu wa Kitengo cha Huduma ya Magereza nchini Kenya.

Kenyatta alimteua Brigedia (Mst) John Kibaso Warioba kama mridhi wa Ogalo na pia kubadilisha Afisa Mkuu aliyesimamia idara za urekebishaji.