Eneo la Mt Kenya litampigia Raila kura hadi mtu wa mwisho- Gavana Nyoro

Muhtasari

•Gavana huyo amesema eneo hilo halitakubali viongozi wanaozua migawanyiko bali badala yake litamchagua Raila ili kuleta utulivu nchini.

•Raila aliandamana na viongozi wengi wa kisiasa kutoka eneo la Mlima Kenya na angalau magavana sita.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga akiwasili Thika Stadium pamoja na Gavana wa Kiambu James Nyoro.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga akiwasili Thika Stadium pamoja na Gavana wa Kiambu James Nyoro.
Image: JAMES MBAKA

Gavana wa Kiambu James Nyoro amesema eneo la Mlima Kenya litampigia kura kinara wa ODM Raila Odinga hadi karibu mtu wa mwisho.

Gavana huyo amesema eneo hilo halitakubali viongozi wanaozua migawanyiko bali badala yake litamchagua Raila ili kuleta utulivu nchini.

Amesema kwamba zaidi ya viongozi 1000 ambao walikutana na Raila hapo awali katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya watakuwa mabalozi wake katika kueneza injili ya Azimio La Umoja.

"Hakuna mtu anayepaswa kutilia shaka uwezo wa aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga  kutwaa urais," Nyoro alisema.

Gavana huyo ambaye alimkaribisha Raila katika uwanja wake wa Kiambu kwa uzinduzi wa kampeni za urais za bosi huyo wa ODM, alisema wakati umefika kwa urais wa Raila.

"Baba amepanda mlima na sasa yuko kileleni, amethibitisha makosa kwa akina Thomas wote wanaotilia shaka," gavana huyo alisema.

Nyoro alizungumza huku Raila akiingia katika uwanja wa Thika ambapo alihutubia mkutano mkubwa na kuzindua azma yake ya urais Agosti 9.

Raila aliandamana na viongozi wengi wa kisiasa kutoka eneo la Mlima Kenya na angalau magavana sita.

Hapo awali waziri mkuu huyo wa zamani alikutana na viongozi na wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni pamoja na magavana James Nyoro(Kiambu), Nderitu Muriithi(Laikipia), Hassan Joho(Mombasa) na Francis Kimemia wa Nyandarua.

Magavana wengine ni pamoja na James Ongwae(Kisii), Anyang Ngong'o wa Kisumu na Cyprian Awiti wa Homa Bay, gavana wa Nakuru Lee kinyanjui, Joseph Ole Lenku wa Kajiado, Cornel Rasanga wa Siaya, Wycliffe Oparanya wa Kakamega, Martin Wambora wa Embu miongoni mwa wengine.