DCI kuwashtaki mameneja wa KPLC kufuatia kupotea kwa umeme nchini

Baadhi ya maafisa walitahadharishwa kuwa nyaya zilikuwa karibu kuanguka lakini walipuuza habari hiyo

Muhtasari

•Kufikia sasa hadi mameneja watano wamehojiwa  kufuatia kuporomoka kwa minara minne katika njia ya usambazaji umeme ya Nairobi-Kiambere.

•Kulingana na timu ya uchunguzi ambayo iliotembelea eneo la minara iliyoporomoka, sehemu ya chini ya minara ya njia za umeme  ilikuwa imeharibiwa.

Njia ya usambazaji umeme ya Kenya ilianguka Januari 11.
Njia ya usambazaji umeme ya Kenya ilianguka Januari 11.
Image: HANDOUT

Maafisa wa upelelezi kutoka Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai wametambua baadhi ya wasimamizi katika Kampuni ya Kenya Power kwa ajili ya kuwahoji na kuwafunguliwa mashtaka kufuatia hitilafu ya umeme nchini kote wiki jana.

Kufikia sasa hadi mameneja watano wamehojiwa  kufuatia kuporomoka kwa minara minne katika njia ya usambazaji umeme ya Nairobi-Kiambere.

Polisi wamepanga kuomba Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuwafungulia mashtaka mameneja hao kwa kosa la  kuhujumu uchumi, kutekeleza majukumu yao pamoja na makosa mengine.

Haya yanajiri baada ya uchunguzi kubaini kuwa minara hiyo minne iliyoanguka ilidhoofishwa kimakusudi kabla ya kuporomoka kwa nyaya hizo na kusababisha kukatika kwa umeme kote nchini.

Zaidi ya hayo, DCI imepata ushahidi unaoashiria kuwa mameneja waliosimamia udumishaji wa laini hizo waliarifiwa kuhusu hali ya zenyewe mnamo Novemba mwaka jana lakini wakakosa kuchukua hatua.

“Wapo mashahidi ambao hata walirekodi hali ya nyaya na minara na kutuma kwa wasimamizi kuwataka wachukue hatua lakini wakakosa. Wanakandarasi wa eneo moja waliona minara hiyo ikipotea na kuwatahadharisha wasimamizi lakini hakuna hatua iliyochukuliwa,” afisa mkuu anayefahamu uchunguzi huo alisema.

Mameneja wakuu akiwemo kaimu meneja mkuu, Wasimamizi wa Mtandao, Mhandisi Mkuu wa usambazaji wa stima nchi nzima, wasimamizi katika kitengo cha Huduma ya Usalama wa nchi nzima, afisa mkuu wa usalama Mkoa wa Nairobi na fundi mmoja wamehojiwa.

Wengine wameitwa kufika mbele ya kamati mnamo Jumatatu Januari 17 kwa ajili ya kuhojiwa.

Kulingana na timu ya uchunguzi ambayo iliotembelea eneo la minara iliyoporomoka, sehemu ya chini ya minara ya njia za umeme  ilikuwa imeharibiwa.

Wachunguzi pia waligundua kuwa mihimili ya kuvuka ilikuwa imeondolewa na kufunguliwa,hali ambayo iliababisha minara ya pembeni kuingia ndani.

"Kwa kuwa minara ya pembeni ilikuwa imeharibiwa, haikuweza kuhimili uzito wa kondakta ambao ni mzito sana na vile vile mnara wenyewe."

Kufuatia tukio la Januari 11, rais Kenyatta aliamuru uchunguzi ufanyike mara moja na hatua kuchukuliwa kuhusu hujuma hiyo.