Miguna aapa kuuza mali yake yote na kukana uraia wa Kenya iwapo Raila atatwaa Urais

Muhtasari

•Amedai kuwa waziri huyo mkuu wa zamani hawezi kushinda uchaguzi wa mwaka huu kwa njia ya kuaminika.

•Amedai kwamba yuko tayari kuuza mali yake yote na kukana uraia wake wa Kenya iwapo aliyekuwa waziri mkuu atatwaa urais baadae mwaka huu

Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018
Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018
Image: MAKTABA

Wakili na mwanasiasa mashuhuri Miguna Miguna amesema hatavumilia tena kuwa raia wa Kenya iwapo kinara wa ODM Raila Odinga atanyakua kiti cha urais katika chaguzi kuu za mwezi Agosti.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Miguna amedai kwamba yuko tayari kuuza mali yake yote na kukana uraia wake wa Kenya iwapo aliyekuwa waziri mkuu atatwaa urais baadae mwaka huu.

Miguna ambaye amekuwa akiishi  Canada tangu mwaka wa 2018 ambapo alifurushwa kutoka nchini anajulikana kuwa na uraia wa Kenya na Canada.

"Ikiwa Raila Odinga atakuwa rais wa Kenya, nitauza mali yangu yote iliyo huko na kuukana uraia wangu" Miguna Miguna ameapa.

Wakili huyo aliyezingirwa na utata mwingi  alifurushwa kutoka nchini Kenya mnamo Machi 2018, miezi michache tu baada ya kumuapisha kinara wa ODM Raila Odinga kama rais.

Miguna amesisitiza kwamba angali anaamini Raila alishinda chaguzi za 2007 na 2017 na ndio maana akakubali kumuapisha. Hata hivyo sasa amedai kuwa waziri huyo mkuu wa zamani hawezi kushinda uchaguzi wa mwaka huu kwa njia ya kuaminika.

“Ndiyo, ninaamini kuwa mdanganyifu @RailaOdinga alishinda uchaguzi wa 2007 na 2017 kwa njia ya kuaminika. Ndiyo maana nilimuapisha. Hata hivyo, ukweli kwamba alishinda uchaguzi 2007 na 2017 haimaanishi kwamba atashinda, au anaweza kushinda 2022. Hawezi kushinda kwa njia ya kuaminika” Miguna amesema.

Siku za hivi majuzi Miguna amekuwa akimkosoa kinara wa ODM Raila Odinga pamoja na rais Uhuru Kenyatta huku akiwashtumu kwa kuzuia kurudi kwake.