Sakaja na Margaret Wanjiru nusra washikane mashati katika mkutano wa Kenya Kwanza

Muhtasari

•Ubabe baina ya wagombea wa kiti cha ugavana kaunti ya Nairobi; Bishop Margaret Wanjiru na seneta Johnson Sakaja umeshuhudiwa Jumanne baaada ya wawili hao kukaripiana wakiwa katika mkutano wa UDA ulioandaliwa katika kaunti ya Nairobi.

• Sakaja na Wanjiru ambao ni wanachama wa mrengo wa Kenya kwanza walikabiliana katika mkutano wa hadhara uliondaliwa katika uwanja wa City park ,mtaa wa Parklands.

Ubabe wa kisiasa baina ya wagombea wa kiti cha ugavana wa kaunti ya Nairobi kwa mrengo wa Kenya Kwanza; Bishop Margaret Wanjiru na seneta Johnson Sakaja umeshuhudiwa Jumanne baada ya wawili hao kukaripiana na kurushiana cheche za maneno wakiwa katika mkutano wa muungano wa Kenya kwanza (UDA/ ANC/ FORD Kenya)  ulioandaliwa katika kaunti ya Nairobi.

Sakaja na Wanjiru ambao ni wanachama wa mrengo wa Kenya kwanza walikabiliana katika mkutano wa hadhara uliondaliwa katika uwanja wa City park ,mtaa wa Parklands.

Wawili hao walitofautiana mbele ya vinara wao naibu rais William Ruto, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula ambao ni viongozi wa UDA, ANC na Ford Kenya katika usanjari huo. Wanjiru anaegemea chama cha naibu rais huku seneta Sakaja akicheza ngoma ya Musalia Mudavadi.

Margaret Wanjiru ambaye alikuwa akiwahutubia wakazi wa kaunti hiyo, alisitisha hotuba yake ghafla na kuanza kujibizana na Sakaja ambaye ndiye alikuwa mfawidhi katika hafla hiyo.

Vurugu ilianza baada ya Sakaja kumkatiza Wanjiru wakati ambapo alikuwa anauza sera zake kwa wananchi, ili kumchagua kama gavana wao, huku Wanjiru akionekana kumzomea seneta huyo kwa hasira nyingi na kuondoka jukwaani.

Kwa upande wake seneta Sakaja alisema alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya baadhi ya vijana waliokuwa wamehudhuria mkutano huo kuanza kuzua rabsha huku akikashifu kitendo hicho na kusema kwamba walimuaibisha.

 “Mmenitia aibu sana. Kama Kenya Kwanza, tunapaswa kumpa kila mtu katika timu yetu nafasi ya kuzungumza. Unapokerwa na muziki unaopigwa kwenye redio, hauharibu umeme, unabadilisha kituo. Ikiwa haupendi kile mtu anachosema, kaa tu,”  alisema Sakaja.