Chris Obure ajiuzulu ,ili kuwania ugavana Kisii

Muhtasari

• Katibu mwandamizi katika wizara ya uchukuzi, Chris Obure amejiuzulu wadhifa wake ili kuwania kiti cha ugavana katika kaunti ya Kisii.

• “Mwaka wa 2013, tulikuwa tunataka gavana wa kuweka mikakati ya maendeleo, naamini Ongwae ametimiza hilo na kwa sasa kaunti ya Kisii inahitaji msimamizi mzuri wa rasilimali,” Obure alisema.

 

Image: FACEBOOK// CHRIS OBURE

Katibu mwandamizi katika wizara ya uchukuzi, Chris Obure amejiuzulu wadhifa wake ili kuwania kiti cha ugavana katika kaunti ya Kisii.

Obure ameondokea majukumu hayo serikalini Jumatano 9/2/2022 akisema kwamba anapania kuvivaa viatu vya gavana wa sasa James Ongwae.

Gavana wa sasa wa kaunti hiyo ya Kisii, James Ongwae anamaliza hatamu yake ya miaka kumi ofisini akiwahudumia wakazi wa eneo hilo.

Chris Obure amekiri kwamba yeye ndiye chaguo teule kuwa gavana wa kaunti ya Kisii kutokana na ukwasi wake katika masuala ya utumishi wa umma.

“Mwaka wa 2013, tulikuwa tunataka gavana wa kuweka mikakati ya maendeleo, naamini Ongwae ametimiza hilo na kwa sasa kaunti ya Kisii inahitaji msimamizi mzuri wa rasilimali,” Obure alisema.

Katibu huyo alikuwa seneta wa kwanza kaunti ya Kisii kati ya mwaka wa 2013- 2017 na pia alikuwa na ushawishi mkubwa kwa chama cha ODM katika eneo hilo, ila mwaka wa 2017 alibwagwa na Ongwae katika kinyang’anyirocha ugavana.

Mwengine aliyejiuzulu ni waziri wa maji Sicily Kariuki ambaye ametangaza kuwa atakuwa anawania kiti cha ugavana katika kaunti ya Nyandarua katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.

Hili linajiri huku watumishi wote wa umma wanaolenga kuwania vyeo mbalimbali wakitarajiwa kujiuzulu miezi sita kabla ya uchaguz mkuu kufanyika.