Sijapewa 'direct ticket' katika UDA - Waiguru

Muhtasari

• Gavana wa kaunti ya Kirinyaga, Ann Waiguru ametupilia mbali madai kwamba amepewa tikiti ya moja kwa moja katika kinyangányiro cha ugavana kaunti hiyo.

• Gavana huyo pia hakukosa kumpigia debe naibu rais Wiliam Ruto, akisema kwamba ndiye anayeelewa shida zao na ana mfumokazi bora wa kuzitatua.

Gavana wa kaunti ya Kirinyaga, Ann Waiguru ametupilia mbali madai kwamba amepewa tikiti ya moja kwa moja katika kinyangányiro cha ugavana kaunti hiyo.

Akizungumza Alhamisi 10/2/2022, Waiguru amesema kwamba kura za mchujo katika chama cha UDA ambazo zimeratibiwa kufanyika mwezi Aprili zitakuwa za huru na haki.

Waiguru amewaambia wapinzani wake kutozingatia madai hayo na badala yake kujiandaa kwa kivumbi hicho ambacho ametaja kwamba kitakuwa huru.

Kiongozi huyo amesema kwamba hakuna kiongozi ambaye amepewa tikiti ya moja kwa moja katika chama cha UDA na kuwaomba wanasiasa kukoma kuendesha propaganda hizo za uongo katika kampeni zao.

“Yeyote ambaye wakenya watamuunga mkono atapewa tikiti. Kwa hiyo nawaomba nyote mfanye kampeni zenu kwa amani,”alisema Waiguru.

Matamshi ya Waiguru yanajiri mwezi mmoja baada ya mwakilishi wa kina mama katika kaunti ya Kirinyaga, Wangui Ngirici kugura chama hicho cha UDA akisema kwamba kulikuwa na visa vya upendeleo kwa baadhi ya viongozi.

Ngirici alikuwa amesema kwamba Waiguru alipewa tikiti ya moja kwa moja na chama na hivo kukosa imani ya iwapo shughuli hiyo ingekuwa ya haki, na badala yake kuamua kuwania ugavana wa kaunti ya Kirinyaga kama mgombea binafsi.

Kabla ya kuondoka kwa Ngirici, naibu rais William Ruto alikuwa amewahakikishia wawili hao kwamba shughuli hiyo ingekuwa ya haki na kwamba hawakupaswa kuwa na shauku yoyote.

Akizungumza katika wadi ya Kanyekini, kaunti ya Kirinyaga, Waiguru amesisitiza kwamba chama cha UDA kitapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao, huku akiwarai wakazi kusapoti chama hicho.

“Kazi yetu inaonekana na kila mtu. Wale wenye macho wataona kazi yetu. Tunauza sera za yale tumefanya na kile tunatarajia kufanya  iwapo tutachaguliwa tena. Wale wanaoeneza mambo ya uongo watashangaa kwa sababu wananchi wanaangali maendeleo waliyofanyiwa,”alisema Waiguru.

Gavana huyo pia hakukosa kumpigia debe naibu rais Wiliam Ruto, akisema kwamba ndiye anayeelewa shida zao na ana mfumokazi bora wa kuzitatua.