Kalonzo kuingia Kenya Kwanza - Mudavadi na Ruto waanzisha mikakati

Muhtasari

• Mudavadi  alifichua kwamba wamo katika harakati za kumshawishi Musyoka kuungana nao.

• Viongozi wa Kenya kwanza wanasema malengo ya Kenya Kwanza yanaambatana na msimamo wa Kalonzo kuwezesha wakenya kujimudu na kujikwamua kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

 

DP Ruto awasili Bomas katika uzinduzi wa azma ya urais wa Mudavadi
Image: Ezekiel Aming'a

Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ameelezea imani yake kwamba kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka atajiunga na muungano wa Kenya Kwanza.

Mudavadi siku ya Jumatano alifichua kwamba wamo katika harakati za kumshawishi Musyoka kuungana nao kwani malengo ya Kenya Kwanza yanaambatana na msimamo wa Kalonzo kuwezesha wakenya kujimudu na kujikwamua kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Vigogo wa Muungano wa Kenya Kwanza, Musali Mudavadi wa ANC, Naibu Rais William Ruto wa UDA na Seneta wa Bungoma Moses Wetangula wa Ford Kenya wana Imani kuwa Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka atafanya uamuzi wa busara kujiuunga na mrengo wa Kenya Kwanza ili kuhakiki maono na maazimio ya kuwaleta wakenya pamoja na kufufua uchumi wa Kenya yanaafikiwa.

Mudavadi amesema kuwa kuna msukumo mkubwa kuwasaka marafiki wapya wa kisiasa kuunga mkono mkondo aliouchukua yeye na Seneta Wetangula kujiunga na naibu wa Rais William Ruto kwenye muungano wa Kenya Kwanza.

Alisema wengi walio na dhana kwamba alifanya umauzi huo kwa ajili ya tamaa na makuu ya kibinafsi hawana ufahamu wa umuhimu wa kuyaweka maslahi ya wakenya mbele pasi na misukumo ya siasa za umaarufu, majigambo na ubinafsi.

Wakati huo huo Mudavadi ameionya serikali kutotumia taasisi kama vile DCI, KRA na EACC kujitafutia umaarufu wa kisiasa na kuwakandamiza wakenya hasa viongozi kwa misingi ya misimamo yao ya kisiasa.

Kinara huyo wa ANC alidai kuwa taasisi zinazostahili kutoa huduma muhimu kwa wakenya zimebadilishwa na kuwa vibaraka vya kuabudu uongozi wa sasa.

Mudavadi alikuwa akizungumza siku y Jumatano katika eneo la Murang’a kwenye kampeni za mrengo wa Kenya Kwanza akiwa ameandamana na Naibu wa Rais William Ruto na Kiongozi wa chama cha Ford Kenya, Moses Wetangula.