Moses Kuria kurejea nchini Jumamosi baada ya kulazwa Dubai miezi mitatu

Hajaweza kutembea vizuri kwa kipindi cha zaidi ya miezi minne.

Muhtasari

•Kuria ambaye amekuwa akiugua kwa kipindi cha miezi mitano anatarajiwa kutua katika uwanja wa ndege wa JKIA mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

•Alisema kwamba amealika wagombeaji wote wa kiti cha urais kwa hafla yake ya shukrani kwa uponyaji.

Image: FACEBOOK// MOSES KURIA

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria hatimaye anatarajiwa kutua nchini siku ya Jumamosi kutoka Dubai ambako amekuwa akipokea matibabu maalum kwa takriban miezi mitatu.

Kuria ambaye amekuwa akiugua kwa kipindi cha miezi mitano anatarajiwa kutua katika uwanja wa ndege wa JKIA mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Kuria amewasihi wafuasi wake kumlaki katika uwanja wa JKIA asubuhi hiyo kabla yao kuambatana hadi uwanja wa Thika ambako hafla kubwa ya maombi itaandaliwa.

"Tukutane Jumamosi tarehe 19 Februari 2022, saa kumi na mbili asubuhi, katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kisha tuendelee hadi Uwanja wa Thika kwa mkutano wa maombi ya shukrani kwa muujiza Wake wa uponyaji" Kuria alisema.

Akiwa kwenye mahojiano ya video na Citizen TV usiku wa Jumatano, Kuria alisema kwamba amealika wagombeaji wote wa kiti cha urais kwa hafla yake ya shukrani kwa uponyaji.

"Nimealika kila mtu, nimealika wagombeaji wote urais. Jukumu langu ni kualika, jukumu lao ni kuhudhuria. Siwezi kasema ni nani atahudhuria na nani atakosa" Kuria alisema.

Katika kipindi cha miezi mitatu ambacho kimepita wanasiasa kadhaa wakuu ikwemo DP William Ruto, Peter Munya, Oscar Sudi,Raila Odinga Jr na wengineo wamemtembelea mbunge huyo katika Hospitali ya Marekani alikokuwa amelazwa.

Mwanasiasa huyo aliruhusiwa kutoka hospitali ya Marekani, jijini Dubai siku ya Jumamosi baada ya kuwa amelazwa kwa miezi kadhaa.

Kuria alifunga safari ya Dubai mwishoni mwa mwaka jana kwa minajili ya kupokea matibabu maalum baada ya kuchomwa na mkeka wa stima kwenye miguu yake.

Kufikia kupona kwake Kuria amefanyiwa upasuaji zaidi ya mara nane katika juhudi za kurejesha afya yake. 

Daktari wa mbunge huyo  alifichua kuwa hajaweza kutembea vizuri kwa kipindi cha zaidi ya miezi minne.