Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Tot anapaswa kukamatwa baada ya shambulio-Matiang'i

Muhtasari
  • Dereva wa basi hilo alifariki papo hapo huku wanafunzi kadhaa na walimu wao wakipata majeraha.
Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang'i
Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang'i
Image: Picha:HISANI

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Tot yuko matatani baada ya wanafunzi kadhaa kujeruhiwa baada ya shambulio la majambazi kwenye basi lao Alhamisi usiku.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i mnamo Ijumaa aliamuru kukamatwa kwa mwalimu mkuu kwa misingi ya uzembe.

Walimu wawili, wanafunzi 13 na dereva, walishambuliwa na watu wenye silaha kwenye barabara ya Arror-Tot eneo la Chesuman huko Kerio Valley, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Wanafunzi hao walikuwa wakitoka katika safari ya kimasomo katika Kaunti jirani ya Baringo walipovamiwa na majambazi hao mwendo wa saa 10:30 jioni.

Dereva wa basi hilo alifariki papo hapo huku wanafunzi kadhaa na walimu wao wakipata majeraha.

CS Matiang’i alisema usimamizi wa shule ukiongozwa na mkuu wa shule ulikiuka sheria za saa za kazi za basi la shule.

"Serikali inajutia shambulio la jana usiku dhidi ya walimu, dereva na wanafunzi wa shule ya upili ya Tot. Shambulio hilo lilitokea saa 10:30 jioni. Kuna sera ya serikali inayozuia usafiri wa mabasi ya shule zaidi ya 6:30pm. Katika tukio la Tot, wasimamizi wa shule walikiuka wazi sera iliyoainishwa,” Matiang’i alisema.

Waziri huyo alizidi kumlaumu mkuu wa shule kwa kutozingatia vitisho vya usalama katika eneo hilo.

Aliamuru mkuu wa shule akamatwe na kushtakiwa kwa kukiuka sera ya 6pm-6am na kwa ‘kuzembea’.

"Kukamatwa zaidi kutafuata baada ya uchunguzi kamili kuhusu suala hilo," alisema.

Matiang’i alikuwa akizungumza katika Shule ya Serikali ya Kenya iliyoko Kabete, Nairobi.