Uvamizi Marakwet: Dereva auawa huku wanafunzi 13 wakijeruhiwa

Muhtasari

• Majambazi walivamia msafara wa mabasi ya shule huko bonde la Kerio na kuua dereva huku wakijeruhi wanafunzi 13 na walimu wawil

• Wavamizi hao waliokuwa wamejihami kwa silaha nzito walivamia basi la shule ya Mogil ambalo lilikuwa likiongoza msafara huo na kumuua dereva wake na kisha kumimina risasi kwa wanafunzi na walimu

Image: HISANI

Majambazi walivamia msafara wa mabasi ya shule huko bonde la Kerio na kuua dereva huku wakijeruhi wanafunzi 13 na walimu wawili, katika kisa ambacho kilitokea usiku wa Februari 17

Baadhi ya waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya Kapsowar wakiwa katika hali mbaya.

Wanafunzi na walimu hao walikuwa wanatoka hafla ya kimasomo katika msafara wa mabasi matatu ya shule za Bonde la Kerio, Mogil na shule ya kutwa ya Tot.

Msafara huo uliviziwa karibu na eneo la shule ya msingi ya Chesuman huko Marakwet magharibi walipokuwa wakielekea katika shule ya Tot iliyopo Marakwet Mashariki.

Wavamizi hao waliokuwa wamejihami kwa silaha nzito walivamia basi la shule ya Mogil ambalo lilikuwa likiongoza msafara huo na kumuua dereva wake na kisha kumimina risasi kwa wanafunzi na walimu waliokuwa kwenye basi hilo bila kubagua.

Kulisikika vilio na kamsa za “Mungu! Mungu! Mungu!" wakati wavamizi hao wakifyatua risasi kwa takribani dakika kumi kabla ya kutokomea kuelekea vichakani.

Hapo ndipo wanakijiji walikimbia hapo na kupata wavamizi wametokomea na kuwasaidia majeruhi kwenda hospitalini.

Kamishna wa kaunti ya Elgeyo Marakwet, John Korir alidhibitisha kisa hicho na kusema kwamba anaongoza vikosi vya usalama kuelekea eneo la tukio ili kuwatafuta majambazi hao.

“Hawa majambazi lazima watafutwe na watiwe mbaroni, vitendo kama hivi ni Zaidi ya kuvumiliwa na hatuwezi kubali waendelee kuuwa watu wetu bila hatia,” alisema aliyekuwa inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinnet alipowatembelea waasiriwa.

Kisa hiki kinatokea wiki tatu tu kabla ya mitihani ya kitaifa kung’oa nanga na tukio hili limezua mtafaruku na wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakaazi ambao wameingiwa na wasiwasi mkubwa kwa visa vya wahalifu hawa ambao wanawalenga watoto.

Gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet, Alex Tolgos ameshtumu kisa hicho na kuitaka serikali kuchukulia suala la usalama katika eneo hilo kwa umakini mkubwa ili kuzima mashambulio ya wavamizi hao ambayo yamegharimu Maisha ya watu 85 chini ya miezi sita.

Serikali imepanga kufanya unyang’anyaji wa silaha kwa lazima kutoka kwa watu wa eneo hilo wanaomizimiliki kinyume cha sheria.

Vikosi vya usalama vilivyotuwa eneo hilo ni kama havijawatia hofu majambazi hao ambao wanaendelea kufanya mashambulizi takribani kwa kila siku.