Sabina Chege alazwa hospitalini, akosa kuhudhuria kesi ya 'wizi wa kura'

Muhtasari

•Sabina alitarajiwa kufika mbele ya kamati ya utekelezaji wa maadili ya uchaguzi ya IEBC asubuhi ya Jumanne.

•Otiende alifahamisha Kamati kuwa wamewasilisha kesi mahakamani ili kutafsiriwa iwapo kamati inayoongozwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati iko na mamlaka ya kuendeleza kesi hiyo.

Mwakilishi wa Wanawake wa Murang'a Sabina Chege
Mwakilishi wa Wanawake wa Murang'a Sabina Chege
Image: TWITTER// SABINA CHEGE

Mwakilishi wa wanawake wa  Murang'a Sabina Chege anataka IEBC kuahirisha kesi inayomkabili ya 'wizi wa kura' akilalamikia afya yake.

Kupitia mawakili wake James Orengo, Otiende Amollo na Martin Aloo, mbunge huyo ameomba IEBC kumpatia tarehe mbadala ya kuhudhuria kesi akitaja kuwa amelazwa katika hospitali ya Nairobi baada ya kuugua.

Sabina alitarajiwa kufika mbele ya kamati ya utekelezaji wa maadili ya uchaguzi ya IEBC asubuhi ya Jumanne.

Wakili Otiende aliwasilisha barua ya Daktari Eric Munene kuthibitisha kuwa Bi Chege anaugua.

"Niruhusu niwasilishe barua ya kuthibitisha kuwa mshukiwa hajiwezi na alilazwa Februari 16 katika Hospitali ya Nairobi," Otiende alisema.

Aliongeza: "Tunaomba tupange upya kesi hiyo hadi lini atapatikana."

Mbunge huyo wa Rarienda alifahamisha Kamati kuwa wamewasilisha kesi mahakamani ili kutafsiriwa iwapo kamati inayoongozwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati iko na mamlaka ya kuendeleza kesi hiyo.

Kamati iliahirisha kikao kwa dakika 15 ili kutafakari masuala yaliyotolewa na mawakili wa Chege

Kamati ya Utekelezaji wa Maadili ya Uchaguzi wiki jana ilimwagiza Chege kufika mbele yake kufuatia matamshi yake kuhusu matokeo ya urais ya uchaguzi wa 2017.

Huku akiwataka wakazi kujiandikisha jkama wapiga kura kwa wingi  ili waweze kumpigia kura kinara wa ODM Raila Odinga, Chege aliishia kusema;

"Kule central nimeskia hapawengine wakisema hapa tuliwaibia, kuna kaukweli kidogo. Lakini mjue kama tulijua kuiba si. ata hii tutafanya nini...alafu…alafu."

Chege alifika mbele ya kamati hiyo ya IEBC wiki jana kabla ya kikao kingine kuagizwa asubuhi ya leo (Jumanne).