Ruto awasili Marekani, orodha ya viongozi wakuu walioandamana naye

Muhtasari

•Ruto anatarajiwa kuwa nje ya nchi kwa ziara ya siku kumi na mbili nchini Marekani na Uingereza.

•Seneta wa Nairobi Johnstone Sakaja anaripotiwa kuondoka nchini siku chache zilizopita ili kutayarisha makaribisho ya wajumbe hao wa Kenya Kwanza.

Image: FACEBOOK// DENNIS ITUMBI

Naibu Rais amewasili nchini Marekani kwa ziara ya siku kadhaa kabla ya kuelekea Uingereza.

Ruto ambaye alikuwa ameandamana na kundi la wajumbe wakiwemo wanasiasa  tajika wanaoegemea muungano wa Kenya Kwanza aliwasili  Marekani  muda mfupi baada ya usiku wa manane.

Habari za kuwasili kwa naibu rais zalithibitishwa na mtaalamu wake wa masuala ya kidijitali Dennis Itumbi.

"Naibu Rais William Samoei Ruto awasili Washington-Marekani" Itumbi alitangaza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii. 

Mapokezi ya mgombeaji huyo wa kiti cha urais katika uchaguzi wa mwezi Agosti hayakuwa makubwa .

Ruto anatarajiwa kuwa nje ya nchi kwa ziara ya siku kumi na mbili nchini Marekani na Uingereza.

Aliondoka nchini asubuhi ya Jumapili akiandamana na wajumbe mbalimbali wakiwemo kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, gavana wa Turkana Josephat Nanok, gavana Salim Mvurya wa Kwale, gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru,mtaalamu wake wa mahusiano ya kigeni Ababu Namwamba, kiongozi wa mawasiliano yake Hussein Mohamed na mwanauchumi David Ndii.

Seneta wa Nairobi Johnstone Sakaja anaripotiwa kuondoka nchini siku chache zilizopita ili kutayarisha makaribisho ya wajumbe hao wa Kenya Kwanza.

Wajumbe wengine walio kwenye ziara hiyo ni pamoja na;

  • Roselinda Soipan Tuya - Mbunge
  • Owen Yaa Baya - Mbunge
  • Beatrice Kahai Adagala - Mbunge
  • Alice Wahome - Mbunge
  • Kimani Ichungwa - Mbunge
  • Kipchumba Murkomen - Seneta
  • Augustine Cheruiyot - Mkuu wa Usalama wa Chakula
  • Ali Dau Mohammed - Mshauri Maalum wa Mabadiliko ya Tabianchi
  • Reuben Kirwa Maiyo- Katibu Binafsi wa DP
  • Abdul Khalfan Mwasserah - PAS/COP
  • Abraham Koriri- Mshauri wa Kisheria
  • David Mugonyi - Katibu Mawasiliano
  • Eric Kipkoech - Mwandishi wa hotuba
  • Roseline Tingoi - Katibu Masuala ya Kiserikali
  • William Yampoi - Mkuu wa Usalama
  • Hellen Chepkurgat Samoei -Katibu wa Kibinafsi 
  • Mary Patriciah -Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Utawala