Kalonzo kukutana na Raila asema yupo tayari kuingia Azimio

Muhtasari

• Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka amesema kwamba yupo tayari kuungana na kufanya kazi tena na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

• Alimlaumu Raila Odinga kwa kutoheshimu makubaliano yao waliyoafikiana chini ya muungano wa NASA.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka
Image: MERCY MUMO

Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka amesema kwamba yupo tayari kuungana na kufanya kazi tena na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Kalonzo amesisitiza kwamba lazima Odinga atekeleze makubaliano yao ya mwaka wa 2017 ili kutoa mazingira mazuri ya kufanya kazi.

“Tunapoanza mazungumzo mapya ya kisiasa nchini, nimelazimika kutoa taarifa hii baada ya madai kwamba ninachelewa kufanya maamuzi kuhusu upande nitakaoungana nao na kwamba nitakuwa mjinga nikishirikiana na Odinga,” Kalonzo alisema.

Alimlaumu Raila Odinga kwa kutoheshimu makubaliano yao waliyoafikiana chini ya muungano wa NASA.

Aidha kiongozi huyo amefutilia mbali madai kwamba hakuna uhusiano mzuri kati yake na Raila Odinga.

Kalonzo ambaye ameshikilia kwamba  lazima Odinga atimize makubaliano yao, amemtaka rais Uhuru Kenyatta kuongoza kikao cha mazungumzo baina yao.

“Uhuru ndiye rais na ana nguvu, kwa hivyo ataweza kumaliza tatizo hili,” alisema.

Musyoka pia alimlaumu wakili Makau Mutua kwa kudinda kuharakisha mchakato wa kufanya mazungumzo kuhusu makubaliano yao ya mwaka 2017.

“Nimejaribu kwa muda sasa kumshawishi  Makau Mutua kuita mkutano kati yetu ila juhudi zangu zimegonhga mwamba,” Kalonzo alisema.