Mshukiwa mkuu wa NYS Ben Gethi ahukumiwa kifungo cha miaka 5 jela

Muhtasari
  • Gethi alipatikana na hatia siku ya Jumatatu baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha walitenda makosa hayo
  • Hata hivyo, hakimu mkuu Lawrence Mugambi alimuachilia kwa faini mbadala ya Sh4 milioni
Image: Hisani

Mshukiwa mkuu wa NYS Benson Gethi amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kughushi stakabadhi za zabuni za IEBC.

Gethi alipatikana na hatia siku ya Jumatatu baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha walitenda makosa hayo.

Hata hivyo, hakimu mkuu Lawrence Mugambi alimuachilia kwa faini mbadala ya Sh4 milioni.

Kampuni yake, Solarmak Limited, ilikuwa imeshinda zabuni ya kusambaza taa za sola za IEBC zenye thamani ya Sh105 milioni kwa uchaguzi wa 2013.

Gethi alipatikana na hatia Jumatatu pamoja na mkurugenzi mwenza Joyce Makena na hakimu mkuu wa kitengo cha kupambana na ufisadi Milimani Mugambi kwa kughushi nyaraka za zabuni.

Makena pia atatumikia kifungo sawa na Gethi kwa sababu wote walikuwa wakurugenzi katika kampuni hiyo.

Wengine waliohukumiwa pamoja na wawili hao ni wafanyakazi watatu wa zamani wa IEBC Gabriel Mutunga, Kennedy Ochae na Willie Kamanga.

Mugambi alisema Gethi na Makena watabeba mzigo mkubwa kwa sababu wao ndio walipaswa kunufaika na kughushi.

Hata hivyo, alisema hakuna pesa iliyopotea kutokana na kughushi kwa sababu mpango wao ulizuiwa, kabla ya kulipwa pesa zozote.

Maafisa hao wa IEBC walihukumiwa kila mmoja kivyake kwa makosa mawili ambayo walipatikana na hatia.

Mutunga, ambaye mahakama ilisema ndiye mpangaji mkuu, alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh2.8 milioni.

Ochae alipewa adhabu nafuu baada ya mahakama kusema kuwa alitumiwa tu na Mutunga kama mshiriki.

Yeye (Ochae) aliamriwa kulipa faini ya Sh200,000 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Kamanga, ambaye ana umri wa miaka 70, aliamriwa kulipa faini ya Sh800,000 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Gethi, kupitia wakili wake, alikuwa ameomba mahakama imhurumie katika hukumu hiyo.