Raphael Tuju akana madai ya kuwania ubunge wa Lang'ata

Muhtasari

• Tangu aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju atangaze kuondoka kwake katika uongozi wa chama hicho, kumekuwa na semasema nyingi kuhus mipango yake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

• Bango hilo liliashiria kwamba waziri huyo wa awali hatimaye alikuwa ameamua kuwania wadhifa wa ubunge katika eneo la Lang'ata.

Mitandao ya kijamii, KWA HISANI
Mitandao ya kijamii, KWA HISANI
Image: Bango la Raphael Tuju

Tangu aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju atangaze kuondoka kwake katika uongozi wa chama hicho, kumekuwa na semasema nyingi kuhusu mipango yake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Alhamisi, bango lililokuwa na jina la Tuju, nembo za chama cha Jubilee na heshitegi ya Azimio La Umoja lilisambaa katika mitandao ya kijamii.

Bango hilo liliashiria kwamba waziri huyo wa awali hatimaye alikuwa ameamua kuwania wadhifa wa ubunge katika eneo la Lang'ata.

Pesacheck ambayo ni taasisi inayohakikisha kusambazwa kwa taarifa za ukweli miongoni mwa wananchi ilithibitisha kwamba ujumbe kwenye  bango hilo haukuwa wa kweli.

“Tumezungumza na Tuju kufahamu kuhusu jambo hilo na amekana madai hao,” Pesacheck ilisema.

Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha habari siku ya Jumatano, Tuju alisema kwamba bado alikuwa akiwazia ruwaza yake ya kisiasa na hatua atakazozichukua.

Aidha aliongezea kwamba alikuwa anafanya mashauriano kufahamu iwapo atawania kitu cha useneta katika kaunti ya Nairobi au kaunti ya Siaya ambako alizaliwa.

 “Bado nafanya mashauriano, kama mwanasiasa wa muda mrefu siwezi kurupuka kufanya maamuzi kwa kuwa lazima nifanye uamuzi mzuri. Nitakuwa natangaza rasmi uamuzi wangu katika wiki mbili zijazo,” alisema.

Wakenya wameombwa kutoamini habari za mitandao na kusubiria tangazo kutoka kwa Tuju mwenyewe baada ya wiki mbili alizosema.

 

Mitandao ya kijamii, KWA HISANI
Mitandao ya kijamii, KWA HISANI
Image: Bango la Raphael Tuju