Usambazaji wa mafuta haujaathiriwa - KPC yasema baada ya bomba la mafuta kupasuka Kisumu

Muhtasari
  • KPC yatoa taarifa baada ya bomba la mafuta kupasuka Kisumu
  • Irungu alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuchukua tahadhari na kujiepusha na eneo hilo huku KPC ikifanya ukarabati
KPC yatoa taarifa baada ya bomba la mafuta kupasuka Kisumu
Image: FAITH MATETE

Polisi mjini Kisumu wamezingira barabara ya Kondele-Airport bypass baada ya bomba kuu la dizeli kupasuka mafuta yaliyokuwa yakimwagika.

Bomba hilo lililopasuka usiku wa manane limeshuhudia maelfu ya lita za dizeli zikitiririka katika shamba kubwa la Kanyamedha.

Eneo hilo kwa sasa ni eneo lisiloruhusiwa kwenda kwa  umma.

Kampuni ya Kenya Pipeline imesema kuwa usambazaji wa bidhaa za petroli kote nchini na kanda haujaathiriwa.

Katika taarifa Ijumaa, Mkurugenzi Mkuu wa KPC Macharia Irungu alisema nchi ina hisa kote nchini.

"Hata hivyo tunapenda kuwahakikishia umma kuwa tukio hilo halijaathiri upatikanaji wa bidhaa za petroli nchini na kanda. Tuna hisa za kutosha kwa madaraja yote katika bohari zetu kote nchini," alisema.

Irungu alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuchukua tahadhari na kujiepusha na eneo hilo huku KPC ikifanya ukarabati.

"KPC inafanya kazi kwa karibu na Utawala wa Mkoa, OCPD wa Polisi na mashirika mengine husika ya serikali ili kuhakikisha usalama wa umma," alisema.

KPC ilisema mafuta yaligunduliwa kando ya bomba la Sinendet-Kisumu eneo la Kanyamedha, mwendo wa 12:30 asubuhi.

Mafuta hayo yaliwafanya Polisi mjini Kisumu kuzingira barabara ya Kondele-Airport bypass ili kuwaepusha wenyeji waliokuwa wamejazana eneo hilo ili kuchota mafuta, yaliyokuwa yakitiririka kwenye mkondo wa karibu na mifereji ya maji.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kisumu Anthony Maina alisema hali ilidhibitiwa baada ya KPC kuzima laini hiyo ili kuepusha hatari yoyote.

Alisema hakuna majeruhi yaliyoripotiwa.

Maina aliongeza kuwa wameanzisha uchunguzi kubaini ikiwa ni ajali au ilisababishwa kimakusudi.