Mwanajeshi atiwa mbaroni kwa kunajisi msichana wa miaka 12, Eldoret

Muhtasari

•Elly Kipkoech alikamatwa alasiri ya Jumapili na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Langas baada ya kutuhumiwa kunajisi mwanafunzi huyo wa shule moja ya msingi katika eneo hilo.

•Kwa sasa matayarisho ya kumshtaki Kipkoech kulingana na taratibu za kijeshi yanaendelea baada yake kutambuliwa na mhasiriwa.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika kaunti ya Uasin Gishu wanamzuilia mwanajeshi mmoja wa KDF kwa madai ya kunajisi msichana wa miaka 12.

Elly Kipkoech alikamatwa alasiri ya Jumapili na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Langas baada ya kutuhumiwa kunajisi mwanafunzi huyo wa darasa la saba katika shule moja ya msingi la eneo hilo.

Kitengo cha DCI kimeripoti kwamba mhasiriwa alifika nyumbani mwendo wa saa moja unusu usiku wa Jumamosi na kufahamanisha mamake kuwa alichelewa kwa kuwa alikuwa amezuiliwa na mwanaume ambaye alimdhulumu.

Mama ya msichana huyo alipomhoji zaidi aligundua matone ya damu kwenye nguo zake za ndani na kumsihi afichue mhalifu aliyetekeleza unyama huo.

Baada ya hapo alipiga ripoti na wapelelezi wa Eldoret wakamtafuta mshukiwa ambaye alikuwa amejificha katika mtaa wa Green Park. 

Kwa sasa matayarisho ya kumshtaki Kipkoech kulingana na taratibu za kijeshi yanaendelea baada yake kutambuliwa na mhasiriwa.

Mshukiwa pamoja na mhasiriwa wake tayari wamefanyiwa vipimo katika hospitali ya Moi Teaching and Referral.

DCI imewaonya wahalifu wanaodhulumu watoto na kuapa kukabiliana nao kisheria  licha ya vyeo vyao.