Polisi anyang'anywa silaha baada ya mfanyibiashara kupigwa risasi Juja

Muhtasari

•Sundir Shah ambaye alikuwa miongoni mwa wakurugenzi tisa wa Ndarugo Plantation 1960 Limited waliokuwa wametembelea shamba hilo Jumamosi alifariki baada ya kupigwa risasi.

•Afisa huyo alisema alirudi nyuma na kuwafyatulia risasi washambuliaji hao mara nane lakini hakupata shabaha yake.

Bunduki
Bunduki
Image: Andrew Kasuku

Afisa mmoja wa polisi anachunguzwa baada  ya mfanyibiashara ambaye alikuwa akilinda kupigwa risasi na kuuawa katika shamba moja huko Juja, Kaunti ya Kiambu.

Sundir Shah ambaye alikuwa miongoni mwa wakurugenzi tisa wa Ndarugo Plantation 1960 Limited waliokuwa wametembelea shamba hilo Jumamosi alifariki baada ya kupigwa risasi.

Wakurugenzi hao walipokuwa katika zaira yao katika shamba hilo walisimama karibu na barabara kuu ya Thika mwendo wa saa saba mchana wakati walivamiwa

Shah alipigwa risasi kwenye kifua na kufariki papo hapo. Mlinzi wa polisi aliyekabidhiwa jukumu la kumlinda mwanawe waziri wa zamani John Michuki alikuwa akiwasindikiza wakurugenzi.

Alikuwa amejihami kwa bastola wakati wa tukio. Timu ya wapelelezi kutoka Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imeanza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

Wakurugenzi na polisi waliripoti kwamba walikuwa wamemaliza ziara yao katika shamba hilo na walikuwa wamesimama mahali ambapo wanaume wawili waliokuwa wamejihami kwa bastola walipowavamia. Inaripotiwa kuwa wavamizi walikuwa wakisafiri kwa pikipiki.

Afisa huyo alisema alirudi nyuma na kuwafyatulia risasi washambuliaji hao mara nane lakini hakupata shabaha yake. Polisi walisema genge hilo "lilimpiga risasi" na kumuua marehemu kabla ya kutoroka.

Timu ya wapelelezi  iliyotembelea eneo la tukio hata hivyo ilisema haikupata katriji zozote zilizotumika kutoka kwa washambuliaji hao.

"Katriji zilizotumika ambazo walipata katika eneo la tukio zilikuwa tu zile zilizofyatuliwa kutoka kwa bastola ya afisa ambaye alikuwa akiwalinda wakurugenzi. Hilo limesababisha hatua yao ya kumpokonya afisa huyo silaha kama sehemu ya uchunguzi,” Alisema mpelelezi.

Silaha hiyo ilipelekwa kufanyiwa uchunguzi wa silaha kabla ya uchunguzi wa maiti ambao umepangwa kubaini ikiwa risasi zilizoua ni tofauti na zile za afisa huyo.

Uchunguzi unanuia kubaini ikiwa risasi zilizoua mfanyibiashara huyo zilifyatuliwa na afisa au washambuliaji hao. Polisi walisema kiini cha shambulio hilo bado hakijajulikana.

Timu ya kuchunguza mauaji inapanga kutembelea tena eneo la tukio pamoja na wakurugenzi na mashahidi wengine kwa upelelezi zaidi na kutafuta vidokezo zaidi ikiwa ni pamoja na katriji zilizotumika ambazo zilikosekana.