Azimio kumteua Uhuru Kenyatta kama mwenyekiti

Muhtasari

• Katika mkutano mkuu unaotarajiwa Jumamosi ukumbi wa KICC, muungano wa Azimio la Umoja unatarajiwa kumteua rais Uhuru Kenyatta kama mwenyekiti huku Raila Odinga akiteuliwa kama mgombea urais.

Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga
Image: Maktaba

Vuguvugu la Azimio la Umoja linapotarajiwa kukongamana Jumamosi hii katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi ili kumidhinisha rasmi kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kama mpeperusha bendera wa mrengo huo kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, fununu zinasema kwamba tayari vyama 15 vimekubali kuhudhuria na kumuidhinisha Odinga kuongoza mrengo huo kuelekea uchaguzi mkuu.

Pia fununu zinasema kwamba licha ya kubainika wazi kwamba Odinga ndiye atakayekuwa mgombea urais kutoka muunano huo, pia pana juhudi za kuhakikisha kwamba kiongozi wa chama cha Jubilee rais Uhuru Kenyatta ambaye anaondoka mamlakani anateuliwa kama mwenyekiti wa vuguvugu hilo la Azimio la Umoja.

Hatua hii imetajwa na wachanganuzi wa kisiasa kwamba iwapo ni kweli basi ni njia moja ya chama cha Jubilee kulenga kusalia na ubabe wa kisiasa hata baada ya uchaguzi huo licha ya kutokuwa na mpeperusha bendera katika uchaguzi wa Agosti 9.

Wakati wa hafla hiyo, Kenyatta na Odinga wanatarajiwa kuzindua rasmi muungano wa Azimio la Umoja ambapo rais atakuwa mwenyekiti na Odinga mgombea wa urais. Aidha patakuwa na nafasi nne za manaibu wenyeviti katika mfumo sawa na ule uliotumika na ODM mwaka 2007 wakati wa Pentagon ili kuwa na vigogo kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa vyama vinavyotarajiwa kutiwa saini kubuni rasmi muungano wa Azimio ni DAP-K, Upya, PNU, UPF, NARC, KUP, UDM, DEP, Muungano na PAP.