Vyama 15 vinatarajiwa kumuunga mkono Raila kuelekea Agosti 9

Muhtasari

• Jumamosi itakuwa siku kubwa katika muungano wa Azimio la Umoja huku vyama 15 vikitarajiwa kumzindua rasmi Raila Odinga kama mgombea urais wa vuguvugu hilo.

KInara wa ODM Raila Odinga
Image: George Owiti

Macho yote Jumamosi hii yataelekezwa katika ukumbi wa kimataifa wa KICC jijini Nairobi ambapo fununu zinasema takribani vyama 15 vya kisiasa vinatarajiwa kutangaza rasmi kujiunga katika muungano wa Azimio la Umoja na kumuunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga kama mgombea urais kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Hafla hiyo pia inatazamiwa kuona vyama hivyo vyote vitatia saini ya makubaliano baina ya ODM na Jubilee ambapo itawekwa wazi kwa chama hicho cha serikali kumuunga mkono Odinga kama mpeperusha bendera wa vuguvugu hilo.

Maandalizi ya mkutano huo ambao utajumuisha majumbe 20 pekee kutoka kwa kila chama yanaelekea hatua za mwisho huku juhudi za kuhakikisha wanamshawishi kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kujiunga nao zikiwa zimeshika kasi.

Inasemekana kwamba Alhamis Odinga alifanya kikao cha faragha na Musyoka katika mbinu ya kujaribu kumrai kujiunga na Azimio la Umoja licha ya kinara huyo wa Wiper kusimama kidete kwa kumtaka odinga kutii mkataba wa awali baina yao walipokuwa katika vuguvugu la NASA mwaka 2017.

Taarifa zingine zinasema pia baadae jana Kalonzo pia alifanya mkutano faraghani na kinara wa KANU Gideon Moi na mwanawe rais wa tatu Mwai Kibaki, Jimmy Kibaki katika kile kinachotajwa kuwa ni muendelezo wa kumshawishi Kalonzo kujiunga na Azimio la Umoja.

Hili linakuja siku mbili tu baada ya mwenyekiti huyo wa KANU Gideon Moi kujumuika na Raila katika kampeni za Azimio katika kaunti ya Samburu huku akidokeza kwamba wao kama KANU wamo tayari kuingia katika mrengo wa Azimio

Mwenyekiti wa kamati ya kiufundi ya kampeni za muungano wa Azimio la Umoja ambaye pia ni gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi ametaja mkutano wa Jumamosi kuwa ambao utatoa mwelekeo rasmi kuelekea uchaguzi wa Agosti 9.