MCAs 30 wa Kiambu wagura Jubilee na kujiunga na UDA

Muhtasari

•Wajumbe hao wakiongozwa na spika wa kaunti Stephen Dichu walipokewa kwenye chama cha UDA  na Ruto siku ya Jumamosi nyumbani kwake Karen.

•Haya yanajiri siku moja tu baada ya Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi kuungana tena na Naibu Rais William Ruto

Naibu Rais Wiliam Ruto akaribisha wajumbe 30 wa Kiambu kwenye chama cha UDA.
Naibu Rais Wiliam Ruto akaribisha wajumbe 30 wa Kiambu kwenye chama cha UDA.
Image: FACEBOOK// UDA

Wajumbe 30 wa kaunti Kiambu wamegura chama cha Jubilee chake rais Uhuru Kenyatta na kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho kinahusishwa na naibu rais William Ruto.

Wajumbe hao wakiongozwa na spika wa kaunti Stephen Dichu walipokewa kwenye chama cha UDA  na Ruto siku ya Jumamosi nyumbani kwake Karen.

Akiwakaribisha kwenye chama, naibu rais alisema wajumbe hao wanaamini kuwa kunafaa kuwa na mabadiliko ya kiuchumi ya kutoka juu kwenda chini.

"Timu ya Kenya Kwanza inazidi kukua kila siku. MCAs 30 waliochaguliwa katika Kaunti ya Kiambu wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kaunti Mhe Stephen Ndichu wamejiondoa kwenye Jubilee na kujiunga na UDA. Wanaamini kwamba kunapaswa kuwa na mabadiliko mapya ya kujenga uchumi wetu kutoka chini kabisa. Karibuni Hustler Nation!" Ruto alisema

Ujumbe huo uliambatana na picha ya naibu rais akiwa amezungukwa na wajumbe hao.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi kuungana tena na Naibu Rais William Ruto. Maangi alikuwa amemtoroka  Ruto na kuungana na kinara wa ODM Raila Odinga.

Maangi, ambaye amekuwa mwanachama wa ODM tangu Desemba mwaka jana, anataka kumrithi Gavana James Ongwae katika uchaguzi wa Agosti 9, mwaka huu.

Alipokewa na Ruto katika makazi yake rasmi ya Karen, Nairobi siku ya Ijumaa.