Kuria amtaka Martha Karua ajiunge na Kenya Kwanza na kuwa mgombea mwenza wa Ruto

Muhtasari

•Kuria amemtaka Karua kutangaza msimamo wake huku akimsihi achague upande wa naibu rais William Ruto.

•Mbunge huyo ameweka wazi kwamba hata ikiwa Karua hatakubali ombi lake, uhusiano wao mzuri hautaathirika.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria
Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria
Image: MAKTABA

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amemshinikiza kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua kujiunga na vuguvugu la Kenya-Kwanza.

Kupitia taarifa aliyotoa Jumanne, kiongozi huyo wa Chama Cha Kazi (CCK) amemtaka Karua kutangaza msimamo wake huku akimsihi achague upande wa naibu rais William Ruto.

Kuria amempendekeza Karua kuwa mgombea mwenza wa Ruto katika uchaguzi wa mwezi Agosti. Amesema kwamba uongozi wa Ruto-Karua ndio pekee unaoweza kuokoa Kenya.

"Chagua upande mmoja na uvae jezi yako. Ninatazamia kuona tikiti ya Ruto-Karua kuokoa nchi hii kutoka kwa utawala wa milele wa nasaba na kupatia matumaini kwa mamilioni ya watoto ambao walienda shule bila viatu," Kuria alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Mbunge huyo ameweka wazi kwamba hata ikiwa Karua hatakubali ombi lake, uhusiano wao mzuri hautaathirika.