Kiongozi wa wengi Nairobi, Guyo apoteza wanafamilia wanne kwenye ajali ya barabarani

Muhtasari

•Alisema waliofariki ni kaka yake Hassan Borana, 43, mke wa kaka yake Fatuma Hassan Borana, 39, watoto wao wawili Talasso Hassan Borana, 14 na Jamila Hassan, mwenye umri wa miaka 10.

•Guyo alikuwa akielekea Nairobi kutoka Isiolo na alikuwa amekutana na ndugu huyo njiani kabla ya ajali hiyo.

Kiongozi wa Wengi katika kaunti ya Nairobi Abdi Guyo
Kiongozi wa Wengi katika kaunti ya Nairobi Abdi Guyo
Image: Ezekiel Aminga

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Nairobi na ambaye ni MCA wa Matopeni, Abdi Guyo anawaomboleza watu wanne wa familia yake ambao walipoteza maisha katika mbaya ajali ya barabarani iliyotokea kwenye barabara ya Isiolo-Meru.

Guyo alithibitisha kuangamia kwa wanafamilia hao katika ajali hiyo  iliyotokea Jumatatu.

Alisema waliofariki ni kaka yake Hassan Borana, 43, mke wa kaka yake Fatuma Hassan Borana, 39, watoto wao wawili Talasso Hassan Borana, 14 na Jamila Hassan, mwenye umri wa miaka 10.

Ndugu huyo wake na familia walikuwa wakirejea nyumbani kwao Isiolo kutoka Nairobi wakati  ajali ilipotokea.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Subuiga katika Kaunti Ndogo ya Buuri Mashariki, Kaunti ya Meru,  gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Ibrahim.

Lilipata hitilafu ya gurudumu la kulia wakati akiwa barabarani na kusababisha ashindwe kulidhibiti gari hilo.

Gari lilipoteza mwelekeo  na kugonga ukuta. Wanne hao walikufa papo hapo. Mkasa huo ulitokea mwendo wa saa kumi na mbili unusu jioni katika eneo la Maili Saba kando ya barabara ya Meru-Isiolo.

Guyo alikuwa akielekea Nairobi kutoka Isiolo na alikuwa amekutana na ndugu huyo njiani kabla ya ajali hiyo.

Kiongozi huyo wa Wengi Nairobi alitaja kifo cha jamaa zake kama "pigo kubwa" kiasi kwamba hakuweza kuzungumza zaidi.

Mkasa huo ulitokea baada ya Guyo kukaa Isiolo wikendi ambapo aliidhinishwa kuwania kiti cha ugavana na Gavana Mohamed Kuti ambaye alitupilia azma yake ili kumpendekeza. Gavana huyo alitaja matatizo ya kiafya kama sababu za kutotetea kiti hicho.

Guyo alikuwa ameonyesha azma ya kuwania kiti cha Embakasi ya Kati kabla ya kupendekezwa kuwania ugavana wa Isiolo.

(Utafsiri: Samuel Maina)