BBI yazikwa kwenye kaburi la sahau! Mahakama yasema mchakato wa marekebisho ya katiba haukufuata sheria

Muhtasari

• Uamuzi wa mahakama ya upeo unazamisha kabisa matumaini ya kufufua reggae ya BBI

Jaji wa Mahakama ya Juu Philomena Mwilu, Jaji Mkuu Martha Koome, majaji wa Mahakama ya Juu Mohamed Ibrahim na Njoki Ndung'u wakati wa kusikilizwa kwa rufaa ya BBI katika mahakama ya juu Januari 18, 2022. Picha: EZEKIEL AMING'A
Jaji wa Mahakama ya Juu Philomena Mwilu, Jaji Mkuu Martha Koome, majaji wa Mahakama ya Juu Mohamed Ibrahim na Njoki Ndung'u wakati wa kusikilizwa kwa rufaa ya BBI katika mahakama ya juu Januari 18, 2022. Picha: EZEKIEL AMING'A

Mahakama ya upeo imesema kwamba mchakato mzima wa marekebisho ya katiba ulikiuka sheria na kwa hivyo si halali.

Kulingana na uamuzi wa wengi katika mahakama ya upeo msuada wa marekebisho ya katiba hayakufuata kanuni na utaratibu wa sheria.

Akitoa uamuzi wake Jaji Njoki Ndung’u ambaye ndiye wa pekee aliyeunga mkono mchakato wa BBI alisema kuwa Rais Uhuru Kenyatta hakuanzisha mchakato wa marekebisho ya katiba, kupitia Mpango wa BBI. 

Katika uamuzi wake, Jaji Ndung’u hata hivyo alieleza kuwa Rais anaweza kuanzisha mchakato huo kwa wadhifa wake binafsi au rasmi kwa vile amechaguliwa kidemokrasia na Wakenya. 

"Nilisoma kwa makini maamuzi yote, nikitafuta sababu zinazofaa za uamuzi wa kumtenga Rais katika mchakato wa marekebisho na siwezi kupata maelezo yenye mantiki ya kikatiba," alisema. 

Alisema Wakenya wana haki ya kufurahia uwakilishi kutoka kwa viongozi wao waliochaguliwa kihalali, ambao kupitia kwao wanaweza kutumia mamlaka ya kujitawala.

Uamuzi wa mahakama ya upeo unazamisha kabisa matumaini ya kufufua reggae ya BBI.

Katika uamuzi wake siku ya Alhamisi, majaji sita walikubaliana na mahakama kuu na ile ya rufaa kuharamisha mchakato huo.

Walisisitiza kwamba rais Uhuru Kenyatta hana uwezo wa kuasisi mchakato wa kuifanyia katiba marekebisho katika nafasi yake kama kiongozi wa taifa.

Aidha, rais anaweza tu kusimamia mchakato huo kama mkenya wa kawaida tu.

Upande wa rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, ulipewa afasi ya kuwasilisha rufaa katika vipengele saba vilivyotajwa na jaji mkuu Martha koome. 

Jaji mkuu Martha Koome alisema kwamba mahakama hiyo itatoa uamuzi kamili siku ya Jumanne wiki ijayo.