Wanandoa waliouwa mtoto wa miaka 3 huku kakake wa miaka 6 akitazama wakamatwa wakitorokea Tanzania

Muhtasari

•Mwili wa marehemu David ulikuwa na majeraha ya moto kwenye mikono, miguu na matako. Pia ulikuwa na ishara za mateso kwenye shingo, mgongo na uso.

•Mama ya marehemu, Maureen Njoki, alipopokea habari za mauaji ya mwanawe alizichapisha mitandaoni na kusababisha maandamano makubwa ya umma pale.

Washukiwa wa mauaji ya Baby David Ndung'u
Washukiwa wa mauaji ya Baby David Ndung'u
Image: TWITTER// DCI

Polisi wanawazuilia wanandoa wawili wanaodaiwa kutesa mtoto wa rafiki yao hadi kifo kisha kuacha mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mama Lucy.

Phylis Njeri na mumewe Jackson Ngui walikamatwa Alhamisi katika kijiji cha Illasit kilicho karibu na mpaka wa Kenya-Tanzania kufuatia kilio cha umma mitandaoni baada ya ripoti za mauaji ya mtoto David Ndungu ,3, kuibuka.

David anaripotiwa kuuawa kinyama mwezi jana na wanandoa hao waliokuwa wamekabidhiwa jukumu la kumlinda na mamake ambaye alienda Uarabuni Novemba mwaka jana kutafuta riziki.

Washukiwa walitekeleza unyama  huo huku ndugu mkubwa wa marehemu, Peter Ndung'u (6) ambaye pia alikuwa ameachwa mikononi mwao akitazama. Baada ya wanandoa hao kumwangamiza David walimgeukia Peter wakampiga na kumtishia kwa adhabu kali iwapo angeambia yeyote yaliyompata kakake.

Mwili wa marehemu David ulikuwa na majeraha ya moto kwenye mikono, miguu na matako. Pia ulikuwa na ishara za mateso kwenye shingo, mgongo na uso.

Njeri na Ngui walijaribu kumtafutia marehemu huduma za matibabu baada ya kugundua athari za kitendo chao ila tayari alikuwa ashafariki.

Mama ya marehemu, Maureen Njoki, ambaye amekuwa Saudi Arabia kwa takriban miezi minne alipopokea habari za mauaji ya mwanawe alizichapisha mitandaoni na kusababisha maandamano makubwa ya umma pale.

Wapelelezi wa DCI walizindua uchunguzi na kuwakamata washukiwa wakijaribu kutorokea nchi jirani ya Tanzania. Uchunguzi wa awali katika nyumba ya washukiwa ulibaini kuwa David aliuawa ndani ya nyumba kabla ya kutupwa mochari.

Polisi wameanzisha uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo la kukera huku washukiwa wakisubiri kushtakiwa kwa mauaji.