Ruto asema kuporomoka kwa BBI ni mwisho wa utapeli wa siasa

Muhtasari

• Alitaja mipango ya kurekebisha katiba kama ulaghai unaolenga kukidhi maslahi ya ubinafsi wa watu wachache.

• Alifafanua zaidi kwamba nchi imepoteza miaka minne ya thamani katika zoezi lisilofaa ambalo lilivuruga kutekelezwa kwa Ajenda Nne Kuu zan serikali.

• Mwisho wa reggae ni mwisho wa utapeli wa kisiasa nchini Kenya," alisema Ruto.

Image: WILLIAM RUTO TWITTER

Naibu Rais William Ruto amesema kuporomoka kwa kwa mchakato wa BBI kumeashiria mwisho wa utapeli wa kisiasa nchini Kenya.

Alisema uamuzi wa Mahakama ya Juu ni ushindi kwa mamilioni ya Wakenya wanaotatizika kujikimu kimaisha.

Alitaja mipango ya kurekebisha katiba kama ulaghai unaolenga kukidhi maslahi ya ubinafsi wa watu wachache.

"Mwisho wa reggae ni mwisho wa utapeli wa kisiasa nchini Kenya," alisema Ruto.

Alibainisha kuwa uamuzi wa Mahakama ya Juu ulikuwa uthibitisho kwamba BBI ilikuwa kinyume cha sheria na ni zoezi lililokiuka katiba.

Alifafanua zaidi kwamba nchi imepoteza miaka minne ya thamani katika zoezi lisilofaa ambalo lilivuruga kutekelezwa kwa Ajenda Nne Kuu zan serikali.

"Ndugu wa Handshake na waendelezaji wa BBI lazima sasa waombe msamaha kwa Wakenya."

Dkt Ruto alikuwa akizungumza siku ya Alhamisi katika Kaunti za Wajir na Lamu ambako alifanya misururu ya mikutano ya hadhara kupigia debe muungano wa Kenya Kwanza.

Ruto alieleza kuwa Wakenya hawakuwa wajinga kutumiwa vibaya na walio mamlakani.

“Vitisho, vitisho na ushawishi haviwezi kubadilisha nchi. Ni wakati wa viongozi kushindana kwenye jukwaa la masuala na sera,” alisema Naibu Rais.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi alibainisha kuwa Wakenya hawawezi kuendelea kuteseka kwa sababu ya baadhi ya watu wabinafsi na walafi.

"Sasa kwa kuwa BBI ni haramu, wale waliohusika nayo lazima wawajibishwe kwa rasilimali ambazo ziliwekwa katika zoezi hilo la uhalifu," alisema.

Kiongozi wa Chama cha ANC alisema kwamba "hatuwezi kuwa na serikali ambayo daima inawafanyia majaribio watu wa Kenya".

Alieleza kuwa uamuzi wa BBI ni somo kwa mienendo ya uhalifu na kinyume cha sheria inayoshuhudiwa nchini Kenya.

Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula alisema taasisi huru lazima ziheshimiwe na kukataa kutishwa na vibaraka wa serikali wa Serikali.

"Rais lazima afahamu kwamba kila tukio lina matokeo. Wewe (Uhuru) ulishauriwa vibaya, sasa umebeba aibu,” alisema.