Rubis yaahidi kutatua uhaba wa petroli nchini, miezi michache baada ya kushtumiwa kusababisha uhaba huo

Muhtasari

• "Rubis Energy Kenya ingependa kuwajulisha wateja wetu wote kwamba tunajitahidi kutatua tatizo la uhaba wa petroli kwa wepesi mno" sehemu ya waraka wao ilisema

Rubis Energy Kenya
Rubis Energy Kenya
Image: Facebook

Rubis, mojawapo ya kampuni za kuuza na kusambaza kawi nchini imewaahidi Wakenya kuwa na Subira kwani watajitahidi kadri ya uwezo wao kwa kushirikiana na washikadau wengine katika kawi ili kutatua uhaba wa petroli katika maeneo mengi nchini Kenya.

Katika waraka ambao kampuni hiyo iliachia jana kwenye mitandao ya kijamii, walisikitishwa na hali ilivyo nchini ambapo petroli imekosekana, hali ambayo imetatiza shughuli nyingi, sekta ya usafiri ikiwa ndio imelemazwa pakubwa kwani magari hayawezi fanya mizunguko yao pasi na mafuta ya petroli.

“Kuongezeka kwa hivi karibuni kwa bei za petroli katika masoko ya kimataifa kumeathiri na kusababisha ufinyu wa kiuchumi ambapo pia kumeathiri usambazwaji wa bidhaa hiyo. Kwa kushirikiana na mamlaka husika, Rubis Energy Kenya ingependa kuwajulisha wateja wetu wote kwamba tunajitahidi kutatua tatizo la uhaba wa petroli kwa wepesi mno kadri ya uwezo wetu na kulizuia kutoendelea. Tunawashukuru wateja wetu kwa kuwa waelewa na kuwa na ujasiri kwamba tatizo hili litapata ufumbuzi hivi karibuni,” sehemu ya waraka huo ilisoma.

Hii inakuja siku miezi michache tu baada ya katibu wa kudumu katika kitengo cha petroli Andrew Kamau kuteta hadharani kwamba kampuni ya Rubis ilikuwa na njama ya kuhujumu usambazwaji wa bidhaa hiyo nchini kwa kuwekeza katika maghala yao ili kusababisha uhaba bandia wa petroli kote nchini.