Mwanasiasa wa UDA ajeruhiwa baada ya gari lake kumiminiwa risasi 22 Mombasa

Muhtasari

•Tukio hilo wa lilitokea mwendo wa saa nne usiku wa Jumanne na watu. Washambuliaji ambao  walikuwa kwenye magari mawili waliondoka kwa kasi mara baada ya tukio hilo.

•Familia na marafiki zake walisema alikuwa akiendesha gari kutoka msikitini kuelekea nyumbani kwake wakati shambulio hilo lilipotokea.

Mwanasiasa wa Mombasa Ali Mwatsau.
Mwanasiasa wa Mombasa Ali Mwatsau.
Image: HISANI

Polisi jijini Mombasa wanachunguza kisa ambapo mgombeaji kiti cha kisiasa katika eneo bunge la Mvita alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya katika eneo la Tudor.

Gari la mwanasiasa huyo lilimiminiwa takriban risasi 22 akajeruhiwa katika harakati hizo.

Polisi wanasema bado hawajaweza kubaini nia ya kushambuliwa kwa Ali Mwatsau ambaye ni mwanasiasa wa UDA.

Alikimbizwa hospitalini akiwa katika hali nzuri huku msako wa kuwatafuta washukiwa waliokuwa wamejihami kwa bunduki ukiendelea.

Kulingana na polisi, tukio hilo wa lilitokea mwendo wa saa nne usiku wa Jumanne na watu. Washambuliaji ambao  walikuwa kwenye magari mawili waliondoka kwa kasi mara baada ya tukio hilo.

Marafiki wa mwanasiasa huyo walitaja tukio hilo kuwa jaribio la mauaji lisilofanikiwa. Hata hivyo, polisi wameonya dhidi ya uvumi.

Walioshuhudia walisema mhasiriwa alipata majeraha ya risasi mikononi na miguuni na kukimbizwa katika hospitali ya Mombasa kwa matibabu.

Familia na marafiki zake walisema alikuwa akiendesha gari kutoka msikitini kuelekea nyumbani kwake wakati shambulio hilo lilipotokea.

Gari ambalo alikuwa akiendesha wakati shambulio hilo lilipotokea
Gari ambalo alikuwa akiendesha wakati shambulio hilo lilipotokea
Image: HISANI

Polisi walifika katika eneo la tukio na kulivuta gari lililoshambuliwa hadi kituo cha polisi cha eneo hilo.

Mkuu wa DCI katika eneo la Pwani, Washington Njiiru alisema kwamba wapelelezi bado wanakusanya maelezo zaidi kuhusiana na tukio hilo.

"Eneo la tukio lilishughulikiwa na mwanasiasa huyo alipelekwa hospitalini," Njiiru alisema kwa simu.

Mchanganuzi wa masuala ya usalama wa Kisauni na mgombea wa kiti cha MCA cha  Ziwa la Ngombe, Abdallah Abdulrahaman, alivitaka vyombo vya usalama kuharakisha uchunguzi wa shambulio hilo.

“Tunahitaji amani wakati wa uchaguzi huu. Waliohusika wakamatwe,” alisema.