Familia ya Uhuru Kenyatta ilitaka kuniua - Cosmo Choy

Muhtasari

• Cosmo Choy amesema kwamba alitishiwa maisha na familia ya Kenyatta.

• Hatua yake ya kuikosoa serikali na familia ya Kenyatta ilisababisha hali kuwa tete kati ya pande hizo mbili.

Cosmo Choy
Cosmo Choy
Image: Facebook, KWA HISANI

Mchanganuzi na mkosoaji wa masuala ya kisiasa, Cosmo Choy amesema kwamba familia ya rais Uhuru Kenyatta ilikuwa inataka kumuangamiza.

Akizungumza na na mwanablogu wa MGN tv huko Marekani, Choy alisema kwamba mwaka wa 2021 alipaswa kurejea nchini nkuhudhuria mazishi ya mamake mzazi ila akasitisha safari hiyo kwa sababu alipokea habari kwamba kulikuwa na njama ya kumuua.

Cosmo Choi alisema kwamba kosa lake kubwa lilikuwa kusuta visa vya ufisadi vilivyokuwa vinafanikishwa na familia hiyo.

Aliongeza kwamba asilimia kubwa ya kampuni nyingi humu nchini zimetekwa na familia ya rais Uhuru Kenyatta kwa njia ambayo si halali na hivyo kuwaacha wakenya wengi wakihangaika.

Alidokeza kwamba rafiki zake katika idara ya polisi walimtahadharisha dhidi ya kuingia nchini kwani maisha yake yalikuwa hatarini.

"...Mimi sio adui wa polisi wengi walikuwa rafiki zangu, kwa hiyo waliniambia nisiende kwa sababu familia ya Kenyatta ilikuwa inataka kunimaliza," Cosmo Choy alisema.

Aidha, alisema kwamba sababu nyingine ya maisha yake kuwa hatarini ni kwa sababu anaunga mkono naibu rais William Ruto.

Jamaa huyo alishikilia kwamba amesitisha azma yake ya kuwania ubunge katika eneobunge la Embakasi, na kumtaka William Ruto kumtafutia nafasi serikalini pindi atakapoingia ikulu.

Alidai kwamba familia ya rais Kenyatta inapaswa kumuomba msamaha kwa kumsababishia kukosa kuhudhuria maziko ya mamake mzazi.

Choy pia alikana madai kwamba amelipwa pesa na William Ruto ili kumtusi rais Kenyatta na familia yake, akisema kwamba yeye ni mtu anayejituma na kuwa anampenda Ruto kwa utu wake.

Alikata kauli kwamba hawezi kuomba msamaha kwa sababu yeye sio gaidi na hajafanya kosa lolote.