Bitok akataa matokeo ya mchujo wa UDA wa kiti cha ugavana Uasin Gishu

Muhtasari
  • Bitok akataa matokeo ya mchujo wa UDA wa kiti cha ugavana Uasin Gishu
Julius Bitok
Image: MATHEWS NDANYI

Aliyekuwa balozi Julius Bitok amekataa matokeo ya mchujo wa UDA wa kiti cha ugavana katika kaunti ya Uasin Gishu.

Bitok amewasilisha ombi rasmi kwa bodi ya uchaguzi ya UDA kuamuru marudio ya kura ya mchujo haraka iwezekanavyo.

Mwanasiasa Jonathan Bii alitangazwa mshindi kwa zaidi ya kura 71,000 huku Bitok akiibuka wa pili kwa takriban kura 51, 000.

Bitok alisema ana ushahidi kwamba hata kujumlisha kura kuliingiliwa kwa sababu alishinda katika maeneo bunge matano kati ya sita ya kura lakini takwimu zilibadilishwa.

Bitok alisema pia alishambuliwa binafsi na mpinzani wake ambaye pia anafaa kuondolewa kwa msingi wa kuanzisha vurugu.

"Tuna ushahidi wa kuaminika ambao tumekipa chama na tunataka kura za mchujo zirudiwe haraka iwezekanavyo", alisema Bitok.

Alisema karatasi za kupigia kura kwa baadhi ya vituo zilichomwa na wapiga kura na bado chama kilipuuza kitendo hicho na kuendelea na zoezi hilo.

Balozi huyo wa zamani Bitok alisema matumizi ya ghasia na hongo ya wapiga kura pia yameenea sana wakati wa zoezi hilo.

Alihoji ni vipi katika baadhi ya maeneo ya Uasin Gishu waliojitokeza kupiga kura walikuwa zaidi ya asilimia 80 huku waliojitokeza kwa ujumla wakiwa chini ya asilimia 10 kote nchini.

Zaidi ya wawaniaji watano wa ubunge katika eneo bunge la Turbo pia walikataa matokeo ya mchujo katika eneo bunge hilo.

Walidai kuwa matokeo yalibadilishwa.