Spika wa Nairobi Mutura agizwa kufika DCI kwa madai ya wazi

Muhtasari

• "Leo asubuhi nikiwa afisini, afisa fulani alikuja kunikamata bila agizo la kufanya hivyo.

• Mutura si mgeni katika siasa za Nairobi.Kwanza alihudumu kama diwani wa Wadi ya Kimathi kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Makadara katika Uchaguzi Mkuu wa 2013.

• Hata hivyo alipoteza kiti hicho kwa George Aladwa wa ODM katika kura za 2017.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura akiongoza kikao cha mawasilisho mnamo Oktoba 26, 2021 katika vyumba vya bunge. Picha: FI
Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura akiongoza kikao cha mawasilisho mnamo Oktoba 26, 2021 katika vyumba vya bunge. Picha: FI

Spika wa bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura ameagizwa kufika katika afisi za Kurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa madai ya wizi. 

Anatarajiwa kufika katika afisi za DCI  mwendo saa mbili usiku ili kuangazia madai ya wizi. "Nachunguza kuhusu madai ... ya wizi.

Nina sababu za kuamini kuwa wewe, Benson Mutura unahusishwa na kosa hilo au una taarifa ambazo zinaweza kusaidia katika uchunguzi," agizo hilo lilieleza. 

Akizungumza na wanahabari afisini mwake Jumatano, Mutura alisema polisi walijaribu kumkamata katika afisi zake asubuhi. Alitaja jaribio hilo la kukamatwa kama hujuma kwa sababu alitangaza kwamba ataunga mkono azma ya urais ya Naibu Rais William Ruto. 

"Leo asubuhi nikiwa afisini, afisa fulani alikuja kunikamata bila agizo la kufanya hivyo.

Walichokifanya ni kinyume kabisa na kanuni za Kaunti ya Nairobi," alisema. Alisema mara moja alifungwa pingu baada ya kupinga hatua ya maafisa hao.

 "Niko tayari kutii wito. Nimekuwa na uazi katika kile nimekuwa nikifanya," alisema.

Mapema mwezi huu, Spika Mutura alijiunga rasmi na chama cha United Democratic Alliance (UDA).Mutura alisema hagombei kiti chochote cha kisiasa lakini atafanya kazi kwa chama. "Sigombei kiti chochote cha kisiasa. Nitafanya kazi na majukumu nitakayopewa na chama cha UDA,” alisema.

 Mutura si mgeni katika siasa za Nairobi.Kwanza alihudumu kama diwani wa Wadi ya Kimathi kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Makadara katika Uchaguzi Mkuu wa 2013 kwa tikiti ya chama cha TNA. 

Hata hivyo alipoteza kiti hicho kwa George Aladwa wa ODM katika kura za 2017. Alirejea katika uongozi wa jiji mnamo Agosti 14, 2020, baada ya kuchaguliwa kuwa spika wa tatu wa bunge la kaunti.Hii ilikuwa baada ya Beatrice Elachi kujiuzulu kutoka wadhifa huo baada ya mizozo ya muda mrefu na wakilishi wadi.