Uhuru ahudhuria mkutano wa walimu wakuu wa sekondari Mombasa

Muhtasari

• Wakati wa kongamano hilo wajumbe kutoka kaunti zote 47 hutumia fursa hiyo kuwachagua wanachama wa Baraza Kuu la Kitaifa.

• Kongamano hilo linalofunguliwa rasmi leo na Kiongozi wa Taifa ni la 45 tangu lianzishwe.

• Rais Kenyatta ameandamana na Waziri wa Elimu Prof. George Magoha, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amewasili Jijini Mombasa kujumuika na walimu wakuu wa shule kwenye kongamano lao la kila mwaka.

Kongamano hilo ambalo linahudhuriwa na zaidi ya wajumbe 10,000 kutoka kote nchini linafanyika katika ukumbi wa Sheikh Zayed huko Bombolulu, Kisauni. 

Kongamano hilo lilianza tarehe 18 na litamalizika tarehe 22 mwezi huu wa Aprili.

Wakati wa kongamano hilo wajumbe kutoka kaunti zote 47 hutumia fursa hiyo kuwachagua wanachama wa Baraza Kuu la Kitaifa.

Kongamano hilo linalofunguliwa rasmi leo na Kiongozi wa Taifa ni la 45 tangu lianzishwe.

Kikiwa na matawi katika kila kaunti nchini, chama cha walimu wakuu wa shule za umma na zile za kibinafsi hutumia jukwaa hilo kupigia debe majukumu na haki za wanachama kwa manufaa ya sekta ya elimu.

Rais Kenyatta ambaye amewasili huko Bombolulu saa sita ameandamana na Waziri wa Elimu Prof. George Magoha, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho pamoja na maafisa wengine wakuu serikalini.

Litakapokamilika, wanachama watakuwa wamepashwa ufahamu zaidi kuhusu jinsi ya kuendeleza elimu hususan wakati huu ambapo taifa linatekeleza mtaala mpya wa elimu unaozingatia maarifa ya wanafunzi na kuwaanda vyema kwa mahitaji ya kijamii, kiuchumi na teknolojia.