Jimmy Kibaki asema bado hajafikwa na hali halisi ya kifo cha babake

Muhtasari

Jimmy alifichua kuwa kufiwa na babake si jambo rahisi ikizingatiwa jukumu alilocheza maishani mwake. 

 

Mwanawe marehemu Mwai Kibaki, Jimmy Kibaki akimuamkua naibu rais William Ruto 25/04.3022. PICHA;DPPS
Mwanawe marehemu Mwai Kibaki, Jimmy Kibaki akimuamkua naibu rais William Ruto 25/04.3022. PICHA;DPPS

Mwanawe marehemu Rais Mwai Kibaki Jimmy Kibaki amesema kifo cha babake bado hakijazama akilini mwake. 

Akizungumza katika Majengo ya Bunge siku ya Jumatatu, Jimmy alifichua kuwa kufiwa na babake si jambo rahisi ikizingatiwa jukumu alilocheza maishani mwake. 

"Alikuwa baba na pia alikuwepo sana maishani mwangu. Sidhani kama imenigusa sana kwamba ameenda," Jimmy alisema. 

"Nadhani labda itanipata tutakapomzika huko Othaya Jumamosi kuwa hayupo tena," aliongeza. Jimmy alisema baba yake amekuwa katika maisha yake kwa miaka 59 yote akisema"Kwa kweli nitakosa ulinzi."

 “Unajua baba yako akiwa huko unajiona upo salama lakini sasa ameenda kuwa na Mungu na inabidi tujifunze kuishi na hilo,” Jimmy alisema. 

Jimmy ambaye ni mwana wa kwanza wa marehemu Kibaki alisema idadi kubwa ya Wakenya waliojitokeza kutazama mwili wa marehemu rais Bungeni ni dhihirisho kwamba alikuwa na maana kubwa kwao.

 "Tunatiwa moyo kuona kujitokeza kwa wingi kwa Wakenya. Nadhani aliinua sana maisha ya Wakenya na wako hapa kuonyesha shukrani," Jimmy alisema.

 Alisema Kibaki alienda mbali zaidi ya maisha yake ya kisiasa na alithamini sana familia yake. 

"Mzee kwanza kabisa alikuwa mtu wa familia. Hakuna kilichoingilia maisha yake na familia yake." 

Jimmy alifichua kuwa mwaka wa 2003, mara baada ya kuapishwa kwa babake kama rais wa tatu wa Kenya, maafisa wengi wa serikali hawakuelewa kuwa marehemu rais aliweka familia yake mbele ya maisha ya umma. Alisema ni baada ya kuelewa hilo ndipo walipojifunza kufanya kazi kwa urahisi na rais. 

“Kwa hiyo hata mwaka 2003, wajukuu zake walikuwa Ikulu hata siku za kazi, wakiwa likizo ya shule walikuwa Ikulu. "Hilo labda ndilo ambalo Wakenya hawajui kwa sababu kawaida kwa wanasiasa wengi maisha yao ya kisiasa ndio jambo muhimu zaidi," Jimmy alisema. 

Alisema babake kila mara aliwazia taifa ambalo raia wake wote wanajivunia kuwa Wakenya na wala si wasomi wachache tu.

Jimmy alisema maneno ya babake ni kwamba ni jukumu la kila Mkenya kufanya kazi katika kuleta maendeleo ya nchi. 

"Unajua Wakenya wengi wanafikiri ni jukumu la serikali kufanya kazi kwa ajili ya Kenya huku wao wenyewe wakijifanyia kazi." 

Kulingana na Jimmy, babake hakuwahi kuchukua sifa kwa ukuaji wa uchumi ambao nchi ilishuhudia wakati wa utawala wake.

 "Kila mara alitukumbusha kuwa uchumi wakati wa urais wake ulijengwa na Wakenya, sio yeye. Alikuwa akisema mtu mmoja hawezi kujenga uchumi lakini Wakenya wanaweza kujenga nchi yao." 

Jimmy alisema Mzee Kibaki amekuwa akiugua kwa takriban miaka miwili au mitatu kabla ya kifo chake Ijumaa wiki jana. Alisema miezi mitatu iliyopita kabla ya kifo chake ilikuwa ngumu zaidi lakini mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi katika mwezi uliopita. Kibaki alifariki akiwa na umri wa miaka 90.