Vita vya Ukraine: Urusi yaharibu miundombinu ya reli kuzuia silaha za kigeni kuingia Ukraine

Muhtasari

• Njia za reli pia hutumiwa na raia wanaopita kati ya miji au kujaribu kukimbia maeneo yenye migogoro.

Image: GETTY IMAGES

Urusi iligonga miundombinu ya reli kote Ukraine siku ya Jumatatu kwa lengo la kuzuia usambazaji wa silaha za kigeni, huku Marekani ikitangaza kuwa itatoa silaha zaidi licha ya pingamizi la Moscow.

Takriban watu watano waliuawa na 18 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Urusi katika eneo la Vinnytsia, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine.

Njia za reli pia hutumiwa na raia wanaopita kati ya miji au kujaribu kukimbia maeneo yenye migogoro. Mapema mwezi huu karibu raia 50 - wengi wao wakijaribu kuhamia maeneo salama - waliuawa na shambulio la roketi la Urusi kwenye kituo cha reli huko Kramatorsk.

Kwingineko siku ya Jumatatu, mipango ya njia za kibinadamu kuwaruhusu raia kuondoka kwenye kiwanda cha vyuma huko Mariupol ilishindwa.

Moscow ilisema kutakuwa na usitishwaji wa mapigano karibu na kiwanda hicho mapema alasiri lakini naibu waziri mkuu wa Ukraine alisema hakuna makubaliano yaliyofikiwa na kwamba Urusi inafanya kazi bila maafikiao ya pamoja.

Marekani inataka Urusi 'idhoofishwe'

Image: EPA

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alisema Marekani ilitaka kuona Urusi "ikidhoofika" ili isiwe tishio tena kwa mataifa mengine.

Alikuwa akizungumza nchini Poland siku moja baada ya yeye na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Kyiv.

Marekani ilitangaza nyongeza ya $713m (£559m) ya msaada wa kijeshi kwa serikali ya Ukraine na serikali nyingine 15 washirika wa Ulaya.

Mwandishi wa BBC wa masuala ya ulinzi Jonathan Beale anasema maneno ya Bw Austin yanaangazia ushiriki wa Marekani katika vita vya Ukraine.

Balozi wa Urusi mjini Washington alisema Moscow ilituma barua ya kidiplomasia kutaka kusitishwa kwa usambazaji wa silaha za Marekani kwa Ukraine.