Jamaa awapiga mawe mamake na kakake wa miaka 7 hadi kifo Nairobi

Muhtasari

•David Kimani alitumia mawe kuwapiga wawili hao vichwani na kuwaua nyumbani kwao Jumanne asubuhi.

•Polisi wanashuku mzozo wa kinyumbani ulisababisa tukio hilo lakini uchunguzi zaidi unaendelea.

crime scene
crime scene

Mwanamume mwenye umri wa miaka 23 anazuiliwa  katika kituo cha polisi baada ya kuua mamake na kaka yake wa miaka saba katika kisa kilichotokea eneo la Kamulu, Ruai, Kaunti ya Nairobi.

David Kimani alitumia mawe kuwapiga wawili hao vichwani na kuwaua nyumbani kwao Jumanne asubuhi.

Marehemu walitambuliwa kuwa ni Peninah Njoki Kimani, 43 na Maina Karibu.

Jirani aliyejibu mayowe ya marehemu na kujaribu kusaidia pia aligongwa na mawe na kujeruhiwa vibaya. Amelazwa hospitalini akiwa na majeraha kichwani.

Mkuu wa polisi wa Nairobi James Mugera alisema mshukiwa alikamatwa Jumanne katika shamba lililo karibu na eneo la uhalifu.

Aliongeza kuwa wanashuku mzozo wa kinyumbani ulisababisa tukio hilo lakini uchunguzi zaidi unaendelea.

“Mwanamume huyo pamoja na wengine watafanyiwa vipimo vya afya kabla ya kufunguliwa mashtaka ya mauaji. Tunalichunguza,” alisema.

Kesi za mauaji ya kinyumbani zimekuwa zikiongezeka katika miezi ya hivi majuzi huku mamlaka zikiyahusisha na masuala mbalimbali yakiwemo umaskini.

Kwingineko, watu wawili wanaoshukiwa kuwa majambazi waliuawa kwa kupigwa risasi Jumanne usiku katika eneo la Soweto, Nairobi katika kisa cha ujambazi ambacho hakikukamilika.

Wawili hao walikuwa wamevamia na kuwaibia watu katika eneo hilo huku wakiwa wamejihami kwa bastola ghushi na visa.  Walikuwa pamoja na wengine wawili polisi walipoarifiwa.

Polisi walisema walichukua hatua na kuwaagiza watu hao kujisalimisha bila mafanikio na hivyo kufyatua risasi na kuwaua wawili hao.

Miili ya marehemu  ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti baada ya bastola ya bastola ghushi na upanga uliokuwa na damu kupatikana nao. Mwanaume mmoja aliyekuwa amedungwa kisu na kujeruhiwa alikimbizwa hospitalini.