Kifo! Mwanawe mbunge maalum David Sankok ajiua kwa kujipiga risasi

Mbunge maalum David Sankok
Mbunge maalum David Sankok

Wimbi la simanzi limegubika boma la mbunge maalum David Sankok baada ya mwanawe kujipiga risasi na kujiua nyumbani kwao katika kaunti ya Narok siku ya Jumatatu.

Inasemekana marehemu alitumia bunduki ya babake kujitoa uhai.

Polisi, na familia walisema Memusi Sankok alikuwa mwanafunzi wa kidato cha 4 katika Shule ya Upili ya Kericho.

Maafisa wa DCI walitembelea eneo la tukio kukusanya ushahidi wa kisayansi ili kuanzisha uchunguzi.

Baadaye mwili huo ulitolewa nyumbani.

"Baba hakuwa nyumbani wakati mvulana huyo alijipiga risasi na haijafahamika jinsi alivyoipata bunduki ambayo ingepaswa kulindwa ipasavyo," afisa mkuu anayefahamu kisa hicho alisema.

"Alikuwa na umri wa miaka 15. Alijipiga risasi na kufa nyumbani kwao. Hatujui nia gani, "afisa mwingine alisema.

Duru za familia zilisema kuwa mtoto huyo wa kiume na babake wamekuwa na tofauti kuhusu utendaji wake katika masomo.

Polisi walisema wanachunguza nia ya tukio hilo.