Wapelelezi wamhoji mbunge David Sankok baada ya mwanawe kujipiga risasi

Muhtasari

•Wapelelezi walimtembelea Sankok nyumbani kwake na kumshirikisha katika majadiliano mafupi kuhusu kisa hicho.

•Memusi Sankok, 15, alijipiga risasi kwenye kidevu kwa kutumia bastola ya babake alasiri ya Jumatatu.

Mbunge maalum David Sankok akiwa bungeni
Mbunge maalum David Sankok akiwa bungeni
Image: MAKTABA

Mbunge maalum David Sankok alihojiwa na polisi Jumanne kufuatia madai kuwa mwanawe alijitoa uhai kwa kutumia bastola yake nyumbani kwao Narok.

Maafisa wa DCI kutoka ofisi ya ya Narok walimtembelea Sankok nyumbani kwake na kumshirikisha katika majadiliano mafupi kuhusu kisa hicho.

Polisi walisema walirekodi taarifa yake kwa kuwa ni bunduki yake ilitumika katika tukio hilo.

Maafisa hao pia walitembelea eneo ambalo kijana huyo mwenye umri wa miaka 15 aliripotiwa kujipiga risasi.

Mke wa mbunge huyo, binti yake na wafanyakazi wa nyumbani pia walihojiwa.

Bastola aliyotumia marehemu inazuiliwa na maafisa wa DCI kwa minajili ya uchunguzi wa kitaalamu.

Maafisa hao pia walikagua sefu ambapo bastola aina ya Glock ilikuwa imehifadhiwa kabla ya kijana huyo kuipata na kuitumia kujipiga risasi.

Polisi walisema wanataka kuelewa mazingira ya tukio hilo na kubaini ikiwa wangependelea mashtaka yoyote dhidi ya mbunge huyo.

“Kuna madai ya uzembe lakini ukichunguza unakuta alitumia ufunguo kufungua chumba cha kulala na baadaye sefu ambapo bastola ilikuwa. Ngoja tusubiri tuone jinsi itakavyokuwa,” alisema afisa anayefahamu kuhusu kisa hicho.

Chaguo jingine litakuwa kupendekeza uchunguzi juu ya tukio hilo.

Sankok ni mmiliki wa bunduki aliyeidhinishwa.Mmiliki wa bunduki aliyeidhinishwa anatakiwa kuhakikisha usalama wa bunduki

Memusi Sankok, 15, alijipiga risasi kwenye kidevu kwa kutumia bastola ya babake alasiri ya Jumatatu baada ya kuitoa kwenye sefu katika chumba cha kulala cha babake.

Memusi alikuwa mwanafunzi wa kidato cha 3 katika Shule ya Upili ya Kericho.

Kulingana na familia, mvulana huyo alipaswa kurejea shuleni wiki jana.

Babake marehemu, ambaye alikuwa nje ya nchi, alituma pesa za kugharamia mahitaji yake ya shule.

"Badala ya kuenda shule alitoweka nyumbani na kurudi Jumapili tu. Babake pia alirudi nyumbani Jumapili,” rafiki wa familia alisema.

Kulingana na maafisa, siku ya Jumatatu asubuhi Sankok alimuita mvulana huyo kwa mazungumzo.

Inasemekana kwamba kijana huyo alisisitiza kuwa alikuwa amechoka na shule.

Lakini baada ya mazungumzo ya muda mrefu, alikubali kurudi shuleni Jumanne akiongozana na babake.

"Mbunge huyo anasema aliondoka nyumbani kwake na kuhudhuria mkutano wa kisiasa kwenye hoteli yake iliyo karibu. Mwendo wa saa tisa alasiri, mvulana aliingia kwenye mkoba wa mama, akachukua funguo za chumba cha kulala na sefu. Baada ya kufungua sefu, alichukua bastola ya Glock na kujipiga risasi kwenye kidevu, huku risasi ikitoka kwenye upande wa nyuma wa kichwa,” ripoti ya polisi ilisema.

Maafisa wa upelelezi wakiongozwa na mkuu wa DCI wa Narok Mwenda Ethaiba wanachunguza kisa hicho kinachojulikana kama kujitoa uhai.

Polisi wanasema kesi hiyo itashughulikiwa kwa weledi.