15 miongoni mwao raia wa Tanzania wakamatwa katika msako - Isiolo

Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang'i
Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang'i
Image: Picha:HISANI

Dereva mmoja amepigwa risasi na kujeruhiwa alipokuwa akitoroka polisi waliokuwa wakitekeleza amri ya kutotoka nje katika eneo lenye hali tete ya usalama la Merti kaunti ya Isiolo. 

Polisi walisema kisa hicho kilitokea Jumanne jioni wakati wa amri ya kutotoka nje. 

Amri ya kutotoka nje huanza saa kumi na mbili jioni hadi 6 asubuhi na kufuatiwa na operesheni ya usalama. 

Dereva huyo alikutwa akiwa amebeba watu 15 wakiwemo Watanzania watano. Walikuwa wakiendesha gari kutoka eneo la uchimbaji madini la Kom-Durte polisi waliposimamisha gari hilo. 

Mkuu wa polisi wa eneo la Mashariki Rono Bunei alisema dereva alikaidi maagizo na kulazimisha polisi kufyatulia risasi magarudumu ya gari hilo. 

Kisa hicho kilijiri siku moja baada ya serikali kuamuru kupiga marufuku mara moja shughuli za uchimbaji madini ambazo hazina leseni katika eneo la Kom kaunti ndogo ya Merti. 

Operesheni ya ulinzi inaendelea katika eneo hilo ili kuwaondoa wahalifu waliojificha kwenye migodi. 

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i alisema operesheni hiyo itadumu kwa siku 30 huku huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza muda huo kwenda sambamba na zoezi la kupokonya silaha kulenga bunduki na risasi haramu. 

Alisema Baraza la Usalama la Kitaifa liliamua kuzindua "Operesheni Rejesha Amani Marsabit" kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara ya makabila ambayo yamepinga mipango ya amani na kutokamilika kwa dirisha la siku 30 lililotafutwa na viongozi wa kaunti ili kupata maridhiano.