Mauti ndani ya kanisa huku mtoto wa miaka 4 akifariki baada ya kuanguka kutoka orofa ya 4

Muhtasari

• Mwili wa John Maingi, 35, ulikutwa ukining’inia kwenye paa la Kanisa la Remnants of Church Fellowship, siku ya Jumatano muda mrefu baada ya kujitia kitanzi. 

• Marehemu alikuwa ametumia kitambaa cha meza kujitoa uhai.

• Katika kisa kingine cha kusikitisha mtoto mwenye umri wa miaka minne alifariki kutokana na majeraha aliopata baada ya kuanguka kutoka orofa ya nne katika mtaa wa Kahawa West

Image: HISANI

Mwanamume mmoja alifariki kwa baada ya kujinyonga katika kanisa moja huko Kenol, Kaunti ya Murang’a.  

Mwili wa John Maingi, 35, ulikutwa ukining’inia kwenye paa la Kanisa la Remnants of Church Fellowship, siku ya Jumatano muda mrefu baada ya kujitia kitanzi. 

Polisi walisema mchungaji katika kanisa hilo alikuwa akifungua jengo hilo alipogundua kuwa lilikuwa limefungwa kutoka ndani. Baada ya kusaidiwa na  wananchi kufungua, waligundua mwili huo ukining’inia ndani.

 Marehemu alikuwa ametumia kitambaa cha meza kujitoa uhai. Mwili ulitolewa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.  

Katika kisa kingine cha kusikitisha mtoto mwenye umri wa miaka minne alifariki kutokana na majeraha aliopata baada ya kuanguka kutoka orofa ya nne katika mtaa wa Kahawa West, Nairobi siku ya Jumatano.

Polisi walisema Mark Allan alikuwa akicheza na rafiki zake alipoteleza na kuanguka kwa kichwa. Alipata majeraha mabaya na kukimbizwa hospitalini ambapo alifariki.

Polisi walisema wanachunguza tukio hilo.