Kifo cha mgombea kiti wa UDA katika kaunti ya Elgeyo Marakwet chazua maswali

Muhtasari

•Sawachan alikuwa ameshinda kura za mchujo za UDA na alitakiwa kuwania kiti hicho katika uchaguzi wa Agosti.

•Sawachan alifariki katika hospitali moja mjini Eldoret Jumamosi asubuhi saa chache baada ya kupatikana akiwa amepoteza fahamu kando ya barabara ya Eldoret-Uganda.

Mteule wa UDA Mark Bowen
Mteule wa UDA Mark Bowen
Image: MATHEWS NDANYI

Polisi mjini Eldoret wanachunguza hali iliyopelekea kifo cha mpeperusha bendera ya UDA katika kinyang’anyiro cha mwakilishi wadi ya Sambirir, kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Mteule Mark Bowen almaarufu Sawachan alifariki katika hospitali moja mjini Eldoret Jumamosi asubuhi saa chache baada ya kupatikana akiwa amepoteza fahamu kando ya barabara ya Eldoret-Uganda karibu na tawi la Benki Kuu mjini humo.

Sawachan alikuwa ameshinda kura za mchujo za UDA na alitakiwa kuwania kiti hicho katika uchaguzi wa Agosti.

Msamaria mwema aliyekuwa akipita karibu na eneo la tukio alimpeleka marehemu hospitali usiku wa manane siku ya Ijumaa lakini alifariki saa chache baadaye.

Alikuwa amevunjika miguu na haikufahamika jinsi alivyopata majeraha hayo.

Mbunge wa Marakwet Magharibi William Kisaang ambaye ni binamu wa marehemu alisema wameandikisha ripoti kwa polisi kufuatilia tukio hilo.

Mkuu wa polisi wa Uasin Gishu Ayub Gitonga alisema wanachunguza tukio hilo.

"Marehemu alikuwa na majeraha miguuni na kichwani lakini vitu vyake vyote vilipatikana vikiwa sawa," Kisang alisema.

Aliwataka wakazi wa eneo hilo kuwa watulivu wakati tukio hilo linaendelea kuchunguzwa.

"Tumehuzunishwa na msiba huo na tunaomba Mungu aipe familia nguvu ya kustahimili msiba," Kisang alisema.

Marehemu pia alikuwa mfanyabiashara maarufu mjini Eldoret na Seneta Kipchumba Murkomen alikuwa miongoni mwa waliotembelea familia hiyo kuwapa pole.

"Inahuzunisha tumempoteza kiongozi kama huyo na tunaungana na familia kuomboleza wakati huu mgumu," Murkomen alisema.

Alisema marehemu alikuwa mwanachama wa UDA aliyejitolea na alikuwa akijitolea kila wakati kusaidia watu wengi wasio na uwezo katika eneo hilo.

Naibu Rais William Ruto pia alituma risala za rambirambi kwa familia.

Mwili wake ulipelekwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi kusubiri uchunguzi wa maiti utakaosaidia kubaini chanzo cha kifo chake.

Wanafamilia na marafiki walikutana Eldoret na kueleza kushtushwa na kifo chake. Marehemu alikuwa ameoa na alikuwa na watoto.