Watoto wawili wa familia moja wateketea hadi kifo Homa Bay

Muhtasari

•Watoto hao walikuwa na nyanya yao wakati nyumba iliposhika moto uliowaangamiza usiku wa kuamkia Jumapili.

•Uchunguzi wa polisi wa awali umebaini kuwa gesi hiyo ililipuka baada ya kuvuta moto kutoka kwa jiko

Nyumba ambayo mwili wa watoto iliteketea kwa moto huko Ligodho, Ndhiwa Mei 7,202.
Nyumba ambayo mwili wa watoto iliteketea kwa moto huko Ligodho, Ndhiwa Mei 7,202.
Image: ROBERT OMOLLO

Watoto wawili wa familia moja walifariki baada ya gesi kulipuka  nyumbani kwao  katika kijiji cha Ligodho, eneo bunge la Ndhiwa usiku wa kuamkia leo. 

Watoto hao walikuwa na nyanya yao wakati nyumba iliposhika moto uliowaangamiza usiku wa kuamkia Jumapili.

Inaripotiwa kuwa silinda ya gesi ililipuka kwa sababu ya vali ilikuwa imelegea. 

Inasemekana nyanya wa watoto hao alikuwa amejaziwa mtungi wake wa kilo sita katika kituo cha biashara cha eneo hilo. Marehemu waliungua kiasi cha kutotambuliwa. 

Baada ya kufikisha mtungi ule nyumbani, nyanya huyo aliamua kuandaa chakula cha jioni kwa kutumia jiko kwani gesi ilikuwa imewekwa pembeni. 

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Ndhiwa, Paul Rioba alisema nyanya huyo hakutambua kuwa gesi yake ilikuwa ikivuja. 

Nyanya huyo amekuwa akikaa peke yake lakini mara kwa mara huwa anatembelewa na wajukuu. Watoto hao wana umri wa miaka mitano na mitatu. 

“Mama yao aliondoka nyumbani kwake lakini akawapeleka watoto kwa nyanya yao ili awatunze. Tukio hilo lilitokea wakati nyanya alipokuwa akitayarisha chakula,” Rioba alisema. 

Rioba alisema uchunguzi wao wa awali umebaini kuwa gesi hiyo ililipuka baada ya kuvuta moto kutoka kwa jiko. 

Afisa huyo wa polisi alisema mwanamke huyo mzee alifanikiwa kukimbia baada ya mlipuko huo akiwaacha watoto hao wawili.  

"Alijaribu kurudi na kuwachukua watoto lakini alizidiwa nguvu na moto uliokuwa ndani ya nyumba," alisema. 

Miili yao iliyoungua ilipatikana chini ya meza ambapo walikuwa wamejificha. Rioba alielezea kifo hicho kuwa cha kusikitisha lakini alitoa wito kwa wakazi kuwa waangalifu kila wakati wanaposhughulikia mitungi ya gesi. 

"Tuwe waangalifu tunaposhughulikia mitungi ya gesi ili kuepuka kurudia kwa ajali hizo," aliongeza.

(Utafsiri: Samuel Maina)