Wanamgambo 8 watiwa mbaroni, bunduki 12 na risasi 579 zapatikana Marsabit

Muhtasari

•Walikamatwa kufuatia operesheni 'Rudisha Amani Marsabit' ambayo ilitekelezwa  katika eneo la Marsabit ya kati.

•Polisi wameripoti kuwa bunduki tatu aina ya AK 47, G3 moja, Machine Gun moja na risasi 579 zilipatikana katika operesheni hiy

Image: TWITTER// NPS

Polisi katika kaunti ya Marsabit wanawazuilia washukiwa 8 wanaohusishwa na mashambulio ya kigaidi ambayo yamekuwa yakiendelea katika eneo  hilo.

Wanane hao walikamatwa  Jumanne jioni katika operesheni 'Rudisha Amani Marsabit' ambayo ilitekelezwa  katika eneo la Marsabit ya kati.

Polisi wameripoti kuwa bunduki tatu aina ya AK 47, G3 moja, Machine Gun moja na risasi 579 zilipatikana katika operesheni hiyo. Maganda 66 ya risasi na chupa ya mafuta ya bunduki pia zilipatikaa.

Washukiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa ya kigaidi.

Haya yanajiri huku amri ya kutotoka usiku ikiendelea kutekelezwa katika kaunti hiyo ikiendelea. Kafyu hiyo imeweza kufanikisha utulivu kwa kiwango fulani na kuwezesha maafisa wa usalama kutekeleza operesheni za kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi.

"Tunawapongeza wananchi kwa msaada wanaotoa kwa vyombo vya usalama huku tukijitahidi kurejesha amani na hali ya kawaida katika eneo hilo," Taarifa ya polisi inasoma.

Wiki jana  waziri wa Masuala ya Ndani na Uratibu wa Serikali Fred Matiang'i alitangaza amri ya kutotoka nje usiku kwa kipindi cha  mwezi mmoja katika kaunti ya Marsabit.

Matiang'i alisema kafyu hiyo iliwekwa ili kuruhusu vikosi vya usalama kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea huko.

"Kuanzia saa kumi na mbili jioni leo, tumeweka kaunti nzima ya Marsabit chini ya marufuku ya kutotoka nje kwa siku 30. Amri ya kutotoka nje itakuwa kati ya 6 jioni na 6 asubuhi," alisema.

Matiang'i alisema amri ya kutotoka nje ni kuruhusu vikosi vya usalama kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea huko.

Kafyu iliyowekwa itasalia hadi mwanzo wa mwezi Juni.